

Mabingwa wa Tanzania Bara, Simba pamoja na mabingwa wa Kombe la Kagame, Azam watakuwa na kibarua kizito mbele ya AS Vita, DC Motema Pembe (DR Congo) na Zesco United (Zambia) katika Mashindano ya Kombe la Kagame yatakayoanza kutimua vumbi Julai 7-21 jijini Kigali, Rwanda.Katika mashindano hayo Tanzania itawakilishwa na Azam mabingwa watetezi na Simba bingwa mara sita wa kombe la Kagame.
Katibu mkuu wa Cecafa, Nicholas Musonye amenukuliwa na vyombo vya habari vya Kenya kuwa mashindano ya mwaka huu yatakuwa na timu 18 huku yakichukua wiki mbili.
"Tumepokea uthibitisho kutoka kwa Zesco, AS Vita na Motema Pembe ambao wanataka kweli kushiriki katika mashindano haya,” alisema Musonye.
“Hizi ni timu kubwa na ushiriki wao utazisaidia timu zetu kujiandaa na Mashindano ya CAF msimu ujao," Musonye alikaririwa katika mtandao huo.
Hata hivyo Shirikisho la Soka Rwanda (Ferwafa) wanatakiwa kupata barua rasmi ya kutoka Cecafa ikiwaonyesha kuongezea kwa timu ngeni mwaka huu.
Cecafa Kagame Cup inashirikisha timu kutoka Kenya, Rwanda, Burundi, Djibouti, Eritrea, Sudan, Somalia, Sudan Kusini, Ethiopia, Uganda, Tanzania na Zanzibar.



0 Comments