NAHODHA wa timu ya Taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta, ametamba kuendeleza ubabe dhidi ya timu Ali Kiba katika mechi yao ya hisani, itakayopigwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Samatta na msanii wa muziki, Ali Kiba, wameandaa mechi hiyo kwa lengo la kuchangisha fedha za kusaidia watu wenye mahitaji maalumu pamoja na shule za msingi kupitia mfuko wao wa ‘SamaKiba Foundation’.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Samatta, ambaye anacheza katika kikosi cha Genk nchini Ubelgiji, alisema Kiba ajiandae kuondoka uwanjani kichwa chini baada ya kupokea kipigo cha maana.
Alisema kipigo atakachoshusha ni zaidi ya kile cha mwaka jana cha mabao 4-1, ili kumwonyesha jinsi mpira unavyochezwa na si maneno.
Samatta alisema kikosi chake kimesheheni nyota wenye uwezo mkubwa, pamoja na yeye watahakikisha wanaisulubu timu ya Kiba ambao wamekuwa wakiongea sana nje ya uwanja.
“Mimi siongei sana, shughuli mtaona wenyewe uwanjani mtu atakapopigwa bao nne, sita, ninaomba mashabiki wa soka wajitokeze kwa wingi ili kufanikisha lengo letu, kwani ujio wao ndio muhimu,” alisema Samatta.
Kwa upande wake Kiba, alipoulizwa ataweza kulipa kisasi kwa Samatta, alisema yupo vizuri, huku akitambia nyota wake kama Meddie Kagere kuwa watamtoa kimasomaso.
“Sisi kazi tumemaliza, Samatta na wenzake wajipange, wafahamu kuwa nina Kagere ndani na tumefanya mazoezi ya nguvu kuhakikisha tunamnyamazisha,” alisema Kiba.
Alitaja viingilio vya mchezo huo kuwa mzunguko ni Sh 2,000, VIP B 5,000 na majukwaa maalumu yanayoitwa Champion King na Champion Samatta ni Sh 20,000.
0 Comments