Windows

Sakata la Makambo…Msolla amkalia kooni Zahera




sakata la usajili wa Heritier Makambo kutua Horoya FC limechukua taswira mpya baada ya Mwenyekiti wa Yanga, Mshindo Msolla, kusema kocha wa timu hiyo ya Jangwani, Mwinyi Zahera, atapaswa kuelezea kilichotokea kwa mshambuliaji huyo.

Mshambuliaji huyo wa DR Congo alisajiliwa na Yanga msimu huu lakini juzi alisaini mkataba wa miaka mitatu kuichezea Horoya ya Guinea na kuzua taharuki kwa jinsi usajili huo ulivyokuwa wa ghafla.

Lakini Mwenyekiti huyo amedai kuwa mchezaji huyo bado ni mali yao hadi Juni 30, mwakani na kuongeza kuwa Zahera atapaswa kueleza kilichotokea mpaka kumuuza straika huyo.

Mshambuliaji huyo aliondoka na Zahera kwenda nchini Guinea na kusaini mkataba huo unaodaiwa kuwa na thamani ya shilingi milioni 230, lakini huenda Yanga wakaambulia patupu kutokana na jinsi mchakato huo wa usajili ulivyokwenda kiujanja ujanja.

Kwa mujibu wa Msolla, Zahera aliondoka pamoja na Makambo kwenda kwenye majaribio na si kumuuza kama ilivyoripotiwa na mtandao wa timu ya Horoya.

“Maombi yao ilikuwa aende kufanya majaribio atakapofanikiwa ndio kufanyike mazungumzo, kuhusu kumwona Makambo na jezi tunamsubiri kocha arejee aweze kuuambia uongozi kitu gani kimetokea, lakini sisi kama klabu hatukuwa na ofa yoyote kwa sababu alikuwa anakwenda kwenye majaribio,” alisema Msolla.

Msolla alisema wanamsubiri kocha huyo arejee nchini leo ili aeleze kilichotokea mpaka kumuuza mchezaji mwenye mkataba ambao unamalizika mwakani.

“Akirejea tutajua nini kilichotokea na taratibu zitafanyika, klabu haiwezi kutoa mchezaji ambaye ana mkataba kwa hiyo atatueleza na taratibu zipo zinaeleweka,” alisema Msolla.

“Yote kwa yote tunasema bado ni mali ya Yanga na lazima kocha aje tumsikie. Pia Makambo ana ofa nyingine tatu zimeletwa ofisini, kwa hiyo tutaangalia ni nani ambaye amefuata taratibu na nani ambaye hajafuata,” alisema Msolla.

Mshambuliaji huyo ametumia ukurasa wake wa Instagram kuwaaga mashabiki wa Yanga, akiandika: “Nawapenda mashabiki wa Yanga, kila siku mtabaki katika moyo wangu na chochote kinaweza kutokea.”

Makambo anaondoka baada ya kuifungia Yanga mabao 20, ambapo 16 alifunga katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara na manne ni ya Azam Sports Federation Cup (ASFC).

Post a Comment

0 Comments