LIGI ya Zambia inaonekana kuanza kumfufua upya mshambuliaji wa zamani wa Simba, Laudit Mavugo anayechezea timu ya Napsa Stars baada ya nyota huyo kurudishwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Burundi kwa ajili ya maandalizi ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) zitakazofanyika Misri, Juni.
Mavugo aliwekwa nje ya kikosi cha timu ya taifa ya Burundi kwa muda mrefu kutokana na kiwango duni ambacho alikuwa akionyesha katika kikosi cha Simba iliyoamua kuachana naye kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu msimu huu.
Baada ya kuachwa, Mavugo alijiunga na Napsa ambako amekuwa mshambuliaji chaguo la kwanza na hilo limemshawishi kocha Olivier Niyungeko kumjumuisha kwenye kikosi chake cha awali cha wachezaji 28.
Kipa wa KMC inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara ameendelea kuwamo kikosini kama kawaida lakini jina la mshambuliaji wa Yanga, Amissi Tambwe halijajumuishwa.
Kikosi cha nyota 28 wa Burundi kinaundwa na makipa Jonathan Nahimana (KMC), Justin Ndikumana (Sofapaka) na McArthur Arakaza (Lusaka Dynamos) wakati mabeki ni Omar Moussa (Sofapaka), Omar Ngando (AS Kigali), Rachid Léon Harerimana (AS Kigali), Mukura David Nshimirimana (VS), Amora Christophe Nduwarugira (TB Saad), Abdoul Karim Nizigiyimana (Vipers), Fredrick Nsabiyumva (Jomo Cosmos), Delanys Valentine Adelin na Bembo Leta Joel (Ramsbottom United)
Viungo ni Gael Duhayindavyi (Mukura), Gael Bigirimana (Hibernian), Pierre Kwizerae (Al Oruba), Shassiri Nahimana (Al Mojzel), Francis Mustafa (Gor Mahia), Cedric Amissi (Al Tawoun), Hussein Shabani (Ethiopian Coffee FC), Yusuf Ndayishimiye (Ange Noir)
Washambuliaji waliopo kwenye kikosi hicho ni Saido Berahino (Stoke City), Abdoul Fiston (JS Kabylie), Enock Sabumukama (Zesco United), Selemani Y. Ndikumana (AL Adalah), Mohamed Amissi (Nec Breda), Laudit Mavugo (Napsa Stars) na Elvis Kasomba.
0 Comments