


HATIMAYE Polisi Tanzania nayo rasmi imepanda daraja na kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao baada ya juzi kuwafunga Boma FC mabao 2-1 katika mechi ya Ligi Daraja la Kwanza iliyochezwa kwenye Uwanja wa Chuo cha Ushiriki Moshi mkoani Kilimanjaro.
Ushindi huo wa juzi umewafanya "Maafande" hao wa Polisi Tanzania kufikisha pointi 47 na kuongoza katika Kundi A ikifuatiwa na Pamba FC ya jijini Mwanza ambayo ina pointi 42.
Polisi Tanzania imeungana na Namungo FC ya Lindi kutoka Kundi B ambayo imemaliza mechi zake ikiwa na pointi 49 kupanda daraja.
Katika mchezo wa mwisho wa hatua hiyo ya makundi, Pamba kutoka jijini Mwanza ikiwa ugenini kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha ilitoka dare ya goli 1-1 dhidi ya Arusha FC.
Mechi nyingine zilizochezwa juzi za ligi hiyo ilikuwa ni Geita Gold iliyopata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Arusha United wakati Dodoma FC iliwafungwa Mashujaa FC magoli 2-1 katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Transit Camp nayo ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mgambo Shooting wakati Rhino Rangers ya Tabora ikiwa nyumbani ilitoka sare ya goli 1-1 dhidi ya Green Warriors ya Dar es Salaam.
Hatua inayofuata ni ya mechi za mtoano ambazo zitatoa timu zitakaposhuka daraja na kufahamu timu zitakazopanda daraja kutoka katika Ligi ya Mabingwa wa mikoa maarufu SDL.
22



0 Comments