

Kwa matokeo hayo, yaliifanya Simba ifikishe pointi 78, mbili nyuma ya vinaya Yanga, lakini mabingwa hao watetezi wakiwa na mechi nne pungufu za ligi hiyo inayotarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi huu.
Simba sasa imefanikiwa kuvuna pointi sita katika jiji hilo baada ya Ijumaa iliyopita kuichapa Mbeya City mabao 2-1 kwenye uwanja huo huo, hivyo kuondoka na ushindi kwenye mechi zote mbili.
Lilikuwa ni bao la dakika ya 11 la Okwi ambaye ni mshambuliaji mkongwe wa Simba na Timu ya Taifa ya Uganda (The Cranes).
Bao hilo alilifunga kutokana na mpira mrefu uliopigwa kutoka katikati ya uwanja na kumkuta mfungaji, aliyempiga chenga kipa, Aron Kalambo na kupiga shuti ambalo lilitambaa taratibu wavuni, huku juhudi za mabeki wa Prisons kutaka kuuokoa kushindikana.
Dakika ya 25, Okwi alikosa bao alipounganisha krosi safi kutoka kwa Clatous Chama, lakini shuti lake lilipaa juu la lango wa wapinzani wao.
Kipindi cha pili, Prisons walilisakama lango la Simba kupitia kwa Salum Kimenya, Lambart Subianka, Adam Adam na wengine, lakini juhudi zao ziliishia miguuni kwa mabeki wa wapinzani wao wakiongozwa na Erasto Nyoni na Mohamed Hussein 'Zimbwe Jnr', pamoja na mikono ya mlinda mlando, Aishi Manula.
Ili kulinda bao hilo walilolipata mapema, Kocha wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems, aliamua kumtoa Okwi na kumwingiza Jonas Mkude ili kuimarisha safu ya kiungo na baadaye alimtoa Haruna Niyonzima na nafasi yake kuchukuliwa na Hassan Dilunga wakati Nicolas Gyan akichukua nafasi ya Zana Coulibaly baada ya kuona mashambulizi ya Prisons dakika za mwisho yanapitia upande wake.
Kwa upande wa Prisons, imefungwa mechi mbili mfululizo, kwani Alhamisi ilikiona cha moto ilipochapwa mabao 2-1 dhidi ya Yanga kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, sasa inakamata nafasi ya tisa, ikisalia na pointi zake 42, ikicheza mechi 34 nayo pia ikiwa imebakisha mechi nne, ingawa haiko kwenye tishio la timu zilizo kwenye janga la kushuka daraja.
Simba itarejea jijini leo tayari kuwasubiri Coastal Union kutoka Tanga katika mchezo mwingine wa ligi hiyo utakaochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Uhuru wakati Azam FC leo watakuwa ugenini Shinyanga kuwavaa Stand United.



0 Comments