Simba wamebakiwa na mechi nne ambazo zitakuwa dhidi ya Ndanda, Singida United, Biashara na Mtibwa Sugar.
Katika mechi hizo ili Simba awe bingwa inabidi avune pointi tano ili kufikisha pointi 90 ambazo wapinzani wao Yanga hawatazifikia.
Katika kuhakikisha hilo Simba wameanza kutanguliza mguu baada ha kushinda mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar uliopigwa leo Uwanja wa Uhuru.
Mabao ya Simba yalifungwa na John Bocco, Emmanuel Okwi na Cletous Chama ambayo yaliwafanya timu yao kuvuna pointi tatu na kufikisha pointi 85.
Kocha wa Simba Patrick Aussems alisema matokeo waliyopata katika mechi mbili zilizopita dhidi ya Kagera Sugar na Azam yamewapa mzuka wa kupata ushindi kwenye mchezo wa leo na Mtibwa.
"Tulikuwa na presha baada ya kushindwa kupata pointi katika mechi mbili zilizopita ambazo zilituongezea mzuka wa kupata ushindi katika mechi ya leo," alisema Aussems.
Upande wa kocha wa Mtibwa Zubery Katwila alisema kufungwa kwao ilitokana na kuwaacha wapinzani wao Simba kucheza n kutengeneza nafasi kuliko wao.
"Simba walitengeneza nafasi za kufunga ambazo zilitokana na makosa ya mabeki wangu lakini tumebakiwa na michezo miwili nyumbani tunakwenda kutekebisha makosa ambayo tumeyafanya katika mchezo huu na Simba ili kufanya vizuri nyumbani," alisema Katwila.
0 Comments