Windows

Pogba, Lukaku, Sanchez wapigwa ‘kibuti’ Man Utd



MASHABIKI wa Manchester United wamepiga kura kuhusu uwepo wa mastaa wao, Paul Pogba na Romelu Lukaku ndani ya klabu hiyo na wengi wao wamewapiga kibuti, wakisema kuwa ni bora waondoke zao.

Kura hizo zilizoendeshwa na gazeti la The Sun, zimekuja wakati kocha wao, Ole Gunnar Solskjaer, akiwa tayari ameshawapa taarifa za kupitishwa panga kubwa kwa baadhi ya nyota wa timu hiyo.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, mpaka sasa mashabiki zaidi ya 3,000 wameshatoa mapendekezo yao kuhusu wachezaji wenye majina ambao hatima yao kwenye klabu hiyo ya Old Trafford ipo shakani.

Mashabiki hao walipiga kura zilizowatenganisha wachezaji wanaotakiwa kubaki na wale wa kufungashiwa virago.

Wakianza na Pogba, ambaye alionekana kuwa shujaa, baada ya kuondoka kocha, Jose Mourihno, Desemba mwaka jana, asilimia 52 ya mashabiki hao wanataka kiungo huyo aondoke wakati asilimia 48 tu ndio wanamuunga mkono.

Mashabiki hao wameonesha kuchoshwa na Mfaransa huyo licha ya mabao yake 16 aliyofunga msimu huu. Aidha, asilimia 61 ya mashabiki wa United wanataka Romelu Lukaku aondoke huku asilimia 31 wakitaka abaki.

Mbali na mastaa hao, mwingine anayeonekana kuchukiwa zaidi na mashabiki hao ni Alexis Sanchez, ambaye idadi yao kubwa imepiga kura ya kumtaka kocha Solskjaer amfungashie virago haraka iwezekanavyo.

Taarifa za gazeti hilo zinaeleza kuwa, katika idadi hiyo ya kura, asilimia 89 hawataki kumuona Sanchez msimu ujao wakati wanaomkubali wakiwa ni asilimia 11 tu.

Nyota mwingine ambaye anaonekana kutokubalika kwa mashabiki hao ni Nemanja Matic, ambaye asilimia 55 wanataka aondoke na huku asilimia 45 wakitaka abaki.

Pia katika kura hizo, mashabiki hao wamependekeza mastaa ambao wanataka wabaki klabuni hapo kwa kuwapa asilimia kubwa ya kura.

Wachezaji kama Anthony Martial, aliyepata asilimia 69 za wanaomkubali dhidi ya 31 ya waliomkataa na David De Gea, aliyepata asilimia 83 dhidi ya 17 waliomkataa, wameonekana kutetewa kwa kiasi kikubwa.

Post a Comment

0 Comments