Windows

PIGA MAKOFI TAFADHALI



MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba, jana wamefanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mchezo wa ligi hiyo uliopigwa Uwanja wa Uhuru, jijini Dar es Salaam.

Kwa ushindi huo, Simba wamerejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu wakiwa na pointi 85 baada ya kucheza michezo 34 na kushinda michezo 27 wakitoka sare nne wakifungwa mara tatu na kuwaacha watani wao wa jadi Yanga kwa pointi mbili.

Simba walianza mchezo huo kwa kasi na dakika ya sita mshambuliaji, Emmanuel Okwi, alikuwa kwenye eneo la kuotea, lakini alipingana na maamuzi ya mshika kibendera kwa kuudunda mpira chini na kuonyeshwa kadi ya njano.

Dakika mbili baadaye Simba walikaribia kupata bao lakini Clatous Chama, alipoteza nafasi hiyo, kabla ya Haruna Niyonzima na yeye kupiga shuti lililookolewa na beki wa Mtibwa Sugar, Dickson Daudi.

Simba waliendelea kulisakama lango la wapinzani wao na dakika ya 22, nahodha wa timu hiyo ya Wekundu wa Msimbazi, John Bocco, alipiga krosi na mpira kumkuta Chama aliyepiga shuti likaokolewa na Daud wakati mlinda mlango wa Mtibwa, Shaaban Kado, akiwa ametoka langoni.

Katika dakika ya 33, Bocco aliiandikia Simba bao la kuongoza akitumia vizuri krosi ya Meddie Kagere, baada ya kupiga mpira uliomshinda Kado.

Dakika mbili baadaye, Kagere alikosa bao baada ya kushindwa kuunganisha krosi ya Gyan na kupiga shuti lililokwenda pembeni na timu hizo zilikwenda mapumziko Simba wakiwa kifua mbele.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na kiungo wa Zambia, Chama, aliifungia Simba bao la pili baada ya kumpiga chenga beki wa Mtibwa na kuukwamisha mpira nyavuni.

Kabumbu liliendelea huku Mtibwa wakionekana kusaka bao kwa hali na mali na dakika ya 50, Riphat Khamis, alishindwa kuifungia timu yake bao baada ya shuti lake kugonga mwamba kabla ya Jafar Kibaya, kupaisha shuti lake katika eneo zuri la kufunga.

Mashambulizi yaliendelea na dakika ya 56, Okwi alipachika bao la tatu, baada ya kupokea pasi kutoka kwa Jonas Mkude na kupiga shuti.

Dakika ya 81, Riphat Msuya, aliikosesha timu yake ya Mtibwa bao la kufutia machozi akiwa eneo zuri lakini akapaisha mpira, Simba walijibu shambulizi dakika tatu baadaye lakini mshambuliaji, Adam Salamba, hakuwa makini na kupoteza nafasi hiyo kwa kupiga nje.

Hadi mchezo huo unafika dakika ya 90, Simba walitoka uwanjani wakiwa mbele kwa ushindi huo wa mabao 3-0.

Kikosi cha Simba kiliwakilishwa na Aishi Manula, Nicholas Gyan, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, Yussuph Mlipili, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Clatous Chama, Haruna Niyonzima, John Bocco/Mzamiru Yassin (dk 60), Meddie Kagere/Adam Salamba (dk 72), Emmanuel Okwi.

Wakati Mtibwa Sugar walikuwa ni Shaban Shabani, Salum Kanoniissa, Rashid Cassian, Ponela Dickson Daud,Shabani Nditi,Jafar Kibaya/Salehe Abdallah (70), Ally Yussuph, Riphat Msuya, Salum Kihimbwa, Haruna Chanongo/Ismail Mhesa (dk 62).

Post a Comment

0 Comments