Genk. GENK, mji mdogo katika nchi ya Ubelgiji uliopo kilomita 82 kutoka mji mkuu wa Ubelgiji Brussels. Mara ya mwisho niliwasili hapa jioni moja ya mwezi Machi, mwaka 2016. Mbwana Samatta ‘Samagoal’ alikuwa ana miezi miwili tu tangu awasili kutoka DR Congo alikokuwa akichezea klabu ya TP Mazembe.
Wakati huo hakuwa staa mkubwa. Alikuwa ameacha jina kubwa nchini Congo. Safari hiyo, kwa mara ya kwanza katika maisha yake, alikuwa ana kazi ya kutangaza jina lake Ulaya. Kifupi alikuwa na kazi mbili. Kwanza ilikuwa ni kutangaza jina lake, lakini pili kumpiku mshambuliaji nyota wa Ugiriki, Nikos Karelis.
Kilichofuata baada ya hapo ni historia. Historia ya Mtanzania wa kwanza kutamba Ulaya kwa kiasi kikubwa na kukaribia kabisa kuwa mfungaji bora katika Ligi Kuu ya Ubelgiji. Miaka mitatu baadaye, wiki mbili zilizopita niliwasili tena Genk kumfuatilia Samatta. Ndiyo, Samatta yule yule ambaye nilimuacha akiwa mnyonge katika kucha za wenzake ambao tayari walishazoea kucheza Ulaya.
Safari hii nilimkuta Samatta aliye tofauti. Samatta aliye staa mkubwa. Samatta ana mabao 23 katika Ligi Kuu ya Ubelgiji. Katika pambano dhidi ya Antwerp nililohudhuria huku Samatta akifunga bao lake la 23 ndipo nilipogundua ustaa mkubwa wa Samatta katika klabu ya Genk na kwa wakazi wa Genk pamoja na mashabiki.
Wimbo wa mashabiki dhidi yake unaoitwa Samagoal ndio ambao ni maarufu zaidi. Ni mchezaji pekee, ambaye ana wimbo miongoni mwa wachezaji wa Genk kwa sasa. ‘Sama Sama Sama Samagooooal Samagoooooal la la la la la la’.
Katika pambano hilo dhidi ya Antwerp, naingia katika chumba cha waandishi wa habari na jezi iliyoandikwa Tanzania kifuani na kila mwandishi wa habari anafahamu uwepo wangu. Anajua ni kwa sababu ya Samatta. Wananiuliza maswali mawili matatu kuhusu Samatta. Wanaonekana kupagawa na kiwango chake cha ufungaji.
Ndani ya uwanja wakati akiingia uwanjani kupasha misuli yake moto, mashabiki walikuwa wakiimba ‘Sama Sama Samagoal, Samagoaaal, Samagoal’. Napigwa na butwaa. Wakati mechi ilipokuwa ikiendelea Samatta akishika mpira na kufanya vitu vikubwa, mashabiki wanaimba. Alipofunga bao lake maridadi akiwa nje ya boksi la adui na kumwacha kipa, Sinan Bolat akiwa hana la kufanya, mashabiki walilipuka tena na wimbo huo.
Ilinisisimua zaidi wakati alipotolewa katika dakika za mwisho za pambano hilo huku Genk wakiongoza mabao 3-0. Uwanja mzima wa Lumunus Arena ulisimama na kumpa heshima huku wimbo wa ‘Samagoal’ ukirindima.
Aliwapigia makofi mashabiki wa pande zote nne za uwanja na nafasi yake kuchukuliwa na Zinho Gano. Heshima iliyoje. Kijana mmoja mdogo kutoka Mbagala aliyeamua kupambana na maisha yake kupitia kipaji kilichopo katika miguu yake na kichwa chake, hatimaye Wazungu walioujaza Uwanja wa Lumunus Arena walikuwa wamempa heshima yake.
Katika nyumba vya kubadilishia nguo, waandishi wa habari wana hamu ya kuongea na Samatta. Bao lake la 20 la msimu!. Wamepita mastaa wengi Genk ambao kwa sasa wanatamba kwingineko. Akina Christian Benteke, akina Kevin de Bruyne, akina Kalidou Koulibaly na wengineo. Lakini, kwa hawa waliopita katika kizazi hiki, Samatta amefanya mambo makubwa zaidi.
Waandishi wanamuuliza Samatta maswali mengi kuhusu kiwango chake cha kusisimua. Wanamuuliza kuhusu matarajio ya ubingwa (kabla hawajachukua juzi Alhamisi). Anawajibu kwa akili kama ambavyo wachezaji wengine mastaa wa Ulaya wanajibu.
Rafiki yake wa karibu, beki wa kimataifa wa Ghana, Joseph Aidoo ‘Boboo’ anapagawa kwa kuropoka kwa nguvu mbele ya waandishi wa habari wakati Samatta anahojiwa ‘He is goal machine, he is goal machine, he is goal machine’ akimaanisha kwamba, Samatta alikuwa mtambo wa mabao.
Nje ya Uwanja wa Lumunus wachezaji huacha magari yao ya kifahari hapo. Ni utaratibu kwa wachezaji wa Genk kuaacha magari yao nje ya uwanja huo na kisha kupanda basi la pamoja hadi klabuni kwao kula pamoja na kujiandaa na mechi. Baadaye wanarudi hapo na basi na baada ya mechi kila mmoja anaondoka na gari lake binafsi.
Mashabiki wanalijua gari la kifahari aina ya Range Rover ambalo Samatta anaendesha. Nje ya uwanja mashabiki wanalizunguka gari la Samatta na kuomba kupiga naye picha. Ni kitu cha kawaida. Watoto hawaamini wanachokiona. Mashabiki wanaendelea kuimba wimbo wa Samagoal.
Ni mchakato unaochukua zaidi ya saa zima kupiga picha na mashabiki waliopagawa ambao, wanaelekea kuchukua ubingwa kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2011 wakati walipopewa ubingwa wao wa mwisho wa Ligi Kuu ya Ubelgiji na akina De Bruyne.
Tangu kuwasili kwangu Genk mpaka pambano dhidi ya Antwerp likichezwa mbele ya macho yangu nilikuwa sijaongea na Samatta kuhusu umaarufu wake na kazi kubwa aliyofanya kiasi cha kuibuka kuwa staa mkubwa Genk na kisha kutamaniwa na klabu mbalimbali za Ligi Kuu ya England, Hispania na Ujerumani.
Sikutaka kuongea na Samatta mwenyewe kwanza. Nilitaka watu wengine watoa ushuhuda wao kabla ya kuzungumza na Samatta. Unahitaji kusimama kwa nje kwanza ili uione nyumba vizuri zaidi kabla haujaingia ndani.
Je, watu mbalimbali jijini Genk wanazungumziaje kuhusu umaarufu wa Samatta Genk? Mwenyewe anazungumziaje kuhusu hali hiyo? Unafahamu chanzo cha wimbo wa Samagoal? Fuatilia mahojiano haya ya kusisimua kufahamu mengi zaidi, kesho Jumapili.