Mo Dewji awafanyia Saplaizi wachezaji Simba
UKISIKIA jeuri ya fedha ndiyo hii, kwani hata kabla ya msimu wa Ligi Kuu Tanzania Bara haujamalizika, tayari Bilionea wa Simba, Mohammed Dewji `Mo`, ameshaanza kufikiria kuwapiga ‘pamba’ kali wachezaji wake akiamini lazima watatetea ubingwa wao.
Taarifa za uhakika kutoka Simba zinadai kuwa wachezaji hao watatengenezewa suti za kufa mtu ikiwa ni zaidi ya zile walizopewa msimu uliopita wakati wa kugawa tuzo za MO Simba Awards 2018.
Katika msimu huo uliopita, Mo Dewji alitoa tuzo mbalimbali ikiwamo ya kipa bora, beki bora, kiungo bora, mshambuliaji bora, mchezaji bora mwanamke, mhamasishaji bora, tawi bora na mengine.
Taarifa hizo zinadai kwamba, tuzo za mwaka huu zitakuwa ‘bab kubwa’ kulinganisha na msimu uliopita baada ya kufanyiwa marekebisho makubwa ndiyo maana maandalizi yake yanaanza sasa.
“Maandalizi hayo ya tuzo ni kama yameshaanza na nikupe taarifa tu kwamba, wachezaji wetu wameandaliwa suti za aina yake, tunataka msimu huu uwe tofauti na uliopita.
“Hii Mo Dewji Awadrs 2019 itakuwa ya tofauti kidogo ndiyo maana unakuta maandalizi yanaanza mapema, tunaamini ubingwa wa Ligi Kuu tutaupata kwani dalili zimeshaonyesha wazi.
“Ukumbuke kwamba timu yetu imefanya vizuri Ligi ya Mabingwa Afrika tukifika hatua ya robo fainali, hivyo lazima tupongezane na hayo yote yatafanyika kwenye tuzo hizo,” alisema kigogo mmoja ndani ya Simba.
Alisema awali malengo yao ilikuwa kufika hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini wachezaji pamoja na benchi la ufundi wakapambana hadi tone la mwisho na kuvuka malengo baada ya kufika robo fainali, ndiyo maana tuzo za msimu huu wanataka ziwe za aina yake.
Katika tuzo za msimu uliopita Aishi Manula aliibuka kipa bora, beki bora akawa Erasto Nyoni, kiungo bora akawa Shiza Kichuya, Emmanuel Okwi akaibuka na tuzo ya mshambuliaji bora, mchezaji bora kijana ni Rashid Juma na mchezaji bora mwanamke akiwa Zainab Rashid Pazzi.
Aliyeibuka mchezaji bora wa mwaka ni nahodha John Bocco, kutokana na mchango wake mkubwa akiwa kama kiongozi wa wachezaji wenzake, huku Hajji Manara akiwa mhamasishaji bora na Ubungo Terminal wakiibuka na tuzo ya tawi bora la msimu.
Dimba
The post Mo Dewji awafanyia Saplaizi wachezaji Simba appeared first on KWATA UNIT SPORTS & ENTERTAINMENT.
0 Comments