Windows

Makambo, Kagere kila mtu kivyake


KUNA vitu vitatu vyenye mvuto mkubwa kuelekea mwishoni mwa msimu wa Ligi Kuu Bara, yaani ubingwa, timu za kushuka daraja na mbio za kiatu cha dhahabu, ambako kinara Meddie Kagere wa Simba na Heritier Makambo wa Yanga wanachuana ile kinoma.


Hata hivyo, buana, nyota wa zamani wamewaangalia nyota hao na kubaini wawili hao hawafanani hata kidogo katika kasi ya kutupia hata kama sehemu ya mabao yao ndani ya ligi hiyo yanafanana.


Kabla ya mechi za jana Alhamisi, Kagere alikuwa ametupia kambani mabao 20, huku Makambo na Salim Aiyee wakifuata nyuma wakiwa na mabao 16 kisha Emmanuel Okwi na John Bocco nao wakiwafuata na mabao yao 14 kila mmoja.


Nyota wa zamani wa klabu hizo kongwe wameamua kumuengua Makambo kwenye tuzo ya Mfungaji Bora sambamba na Aiyee anayekipiga Mwadui kutokana na idadi ya mechi walizobakiwa nazo kabla ya msimu kufungwa, kulinganisha na alizonazo Kagere.


Frank Kasanga ‘Bwalya’ aliyatazama mabao wanayomiliki mastraika wa Ligi Kuu, kisha kumpa moja asilimia 98 Kagere kubeba Kiatu cha Dhahabu mbele ya wapinzani wake.


Bwalya, beki kisiki wa kati wa zamani wa Nyota Nyekundu na Simba, alisema kinachompa nafasi Kagere kutwaa tuzo ni uwezo wa kufunga mabao mawili hadi matatu katika mechi moja, akitolea mfano Simba ilipocheza na Coastal Union, Uwanja wa Mkwakwani staa huyo alifunga mawili, marudiano taifa alifunga matatu (hat-trick).


“Nimemfuatilia Makambo alifunga mabao mawili kwenye mechi moja dhidi ya Mbeya City, lakini kwa asilimia kubwa anafunga bao moja moja, Yanga imebakiza mechi mbili tu, nilitegemea ilipocheza na Ruvu angetupia ili ambane Kagere, ila alichemsha,” alisema.


“Simba imebakiza mechi tano (pamoja na ya jana dhidi ya Mtibwa) katika hizo yoyote anaweza kufanya mambo na kuzidi kuongeza idadi ya mabao ndio maana naamini atatwaa kiatu, Aiyee ni kama kapotea kwa sasa hawezi kumfukuza,” aliongeza Bwalya.


Naye Winga wa zamani wa Yanga, Ally Yusuf ‘Tigana’ alisema kwa mechi tano mkononi ndiko kunakompa nafasi kubwa Kagere kuchukua kiatu cha dhahabu kwa msimu huu “Jamaa ni mpambanaji, ana shauku ya kufunga ndio maana ndani ya dakika 90 hakati tamaa, nampa nafasi kwa sababu anaongoza kwa mabao 20 na mechi walizobakiwa nazo,” alisema Tigana, huku Emmanuel Gabriel straika wa zamani wa Simba, alisema kwa aina ya uchezaji wa Kagere na mechi walizobakia nazo Simba, mkononi alidai anampa nafasi kubwa ya kuchukua kiatu cha dhahabu kuliko Makambo.


“Ingawa kwenye mpira jambo lolote linaweza likatokea, ingependeza zaidi Makambo angefunga dhidi ya Ruvu hapo angempa changamoto Kagere, Yanga wamebakiwa na mechi mbili, ambazo ngumu kwa staa huyo kufikisha mabao 20,” alisema Gabriel.


Aiyee aliyeongoza kwa mabao ndani ya mwaka 2019 alisema; “Tangu mapema nilishawahi kusema straika ninayemhofia ni Kagere kwa sababu Simba walikuwa na mechi nyingi za viporo, lakini pia jamaa ni mpambanaji vya kutosha.”


Post a Comment

0 Comments