


KIKOSI cha Azam tayari kipo mkoani Lindi kwa ajili ya mchezo wao wa fainali ya Kombe la FA (Azam Sports Federation Cup) dhidi Lipuli itakayopigwa kesho Jumamosi, huku benchi la ufundi la timu hiyo likitamba kuwa lazima wafanye mambo Uwanja wa Ilulu.
Kocha Mkuu wa Azam, Meja Mstaafu Abdul Mingange, alisema wamesafiri mapema kwenda Lindi kwa lengo la kuzoea mazingira na kujiweka katika nafasi nzuri ya kukata tiketi ya CAF.
“Hali ya hewa ya Lindi ni tofauti na Dar, hivyo tunaenda mapema ili tuweze kuzoea mazingira mapema, kwani tunahitaji ushindi katika mchezo huu na tumezungumza na vijana kuwaeleza umuhimu wa mchezo huo na wameahidi kufanya kweli,” alisema.
Hata hivyo, nyota wa Lipuli, Paul Nonga alisema mchezo wao dhidi ya Azam utakuwa mgumu kwa vile hata wao wanataka tiketi ya kuwakilisha nchi msimu ujao.
“Unajua katika Ligi Kuu hakuna aliyeibuka mbabe, hivyo fainali hii ya FA ndiyo itakayoamua mkali kwa vile lazima mshindi apatikane na Lipuli tunataka kuandika historia ya kuwakilisha nchi kwa mara ya kwanza,” alisema straika huyo wa zamani wa Yanga.
Nonga aliyezichezea pia Mbeya City na Mwadui, alisema mchezo huo una maana kubwa mbili, kwanza ni kuwa mbabe wa Azam kama wataifunga na kushiriki mechi za kimataifa.



0 Comments