

MANCHESTER, ENGLAND. UMESHAISIKIA hii? Unaambiwa hivi, Sir Alex Ferguson ameripotiwa kumtaka Mauricio Pochettino apewe kazi ya kuinoa Manchester United kuliko Ole Gunnar Solskjaer, ambaye mabosi wa timu hiyo wakemkabidhi kazi hiyo.Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana juzi Jumapili ni kwamba Ferguson alihuzunishwa na kitendo cha mabosi wa timu hiyo kushindwa kumfuata kuomba ushauri juu ya uteuzi wa kocha mpya huko Old Trafford.
Baada ya kufutwa kazi Jose Mourinho, Desemba mwaka jana, Solskjaer alipewa kazi kwa muda, lakini baada ya kufanya vizuri kwenye mechi za awali, mabosi wa timu hiyo waliamua kumpa kibarua cha kudumu hasa baada ya kuitupa nje PSG kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Lakini baada ya Ole kupewa kibarua cha kudumu tu mambo yamebadilika na timu hiyo imechapwa kwenye mechi nane kati ya 12 za mwisho ilizocheza kwenye michuano yote.
Solskjaer alipewa kibarua cha kudumu mwezi Machi, aliposainishwa mkataba wa miaka mitatu akiwa na majukumu ya kuirudisha timu kwenye mstari.
Taarifa zinadai Ferguson alitaka timu hiyo imchukue kocha wa Tottenham, Pochettino kabla hata hawajampa mkataba Solskjaer.
Fergie alisema anavutiwa na Pochettino baada ya kufikisha Spurs kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu akiwa amesajili mchezaji mmoja tu katika madirisha matatu ya usajili.
Kocha huyo mkongwe alisema alihuzunika sana kwa namna Ed Woodward na mabosi wenzake walivyomchunia kwenye suala la kocha mpya kwenye kikosi hicho cha Old Trafford.



0 Comments