MCHEZO wa Leo wa Ligi Kuu England kati ya Manchester United dhidi ya Cardiff utakaochezwa uwanja wa Old Trafford majira ya saa 11:00 utakuwa ni wa mwisho kwa kiungo Ander Herrera na utakuwa ni kwa ajili ya kuwaaga mashabiki zake.
Herrera amethibitisha kuiacha timu yake hiyo ya Manchester United mwisho wa msimu huu baada ya kuitumikia kwa muda mrefu na mkataba wake unatarajia kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni. Anatarajiwa kujiunga na kikosi cha Paris Saint- German (PSG) msimu huu endapo watafanya makubaliano mapema.
Herrera mwenye miaka 29 alijiunga na Manchester United msimu wa mwaka 2014 akitokea kikosi cha Athletic Bilbao na amecheza zaidi ya mechi 189 kwenye kikosi chake hicho.
"Nimeshinda taji Ligi ya Europa, FA na Carabao kwa kipindi nilichokuwa navaa jezi niipendayo ambayo ina mashabiki wengi wakarimu na wenye upendo, nitaikumbuka sana timu yangu sina budi kusema kwa heri," amesema Herrera ambaye ana tuzo ya mchezaji bora wa mwaka msimu wa 2016-17.
0 Comments