

Lipuli imembatiza kwa moto mwenyekiti wa mpya Yanga, Dk Mshindo Msolla baada ya kuichapa timu hiyo kwa mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Samora, mkoani Iringa. Ushindi huo unaifanya Lipuli kufuzu kwa fainali ya Kombe la FA kwa mara ya kwanza itacheza na Azam kwenye Uwanja wa Ilulu, Lindi huku ikiacha majonzi kwa uongozi mpya wa Yanga chini ya mwenyekiti, Msolla.
Mshambuliaji wa zamani wa Yanga, Paul Nonga alifunga bao la kuongoza kabla ya Jimmyshoji Mwasondole kupachika bao la pili na kuizima ndoto ya Yanga kucheza fainali ya Kombe la FA mwaka huu.
Yanga ilianza mchezo huo kwa kusuasua na kuwaacha wenyeji Lipuli kutawala mchezo huo na dakika 27, Nonga alitumia vizuri makossa ya mabeki kufunga goli hilo.
Nonga alifunga akimalizia mpira uliotema na kipa Klaus Kindoki na kupiga shuti lililokwenda moja kwa moja nyavuni.
Yanga ilijaribu kufanya mashambulizi ya hapa na pale huku Heritier Makambo akikosa bao la wazi dakika ya 30 akiwa amebaki yeye na kipa wa Lipuli, Yusuph Mohamed.
Lipuli walipata bao la pili, lililotokana na piga nikupige kati ya mabeki wa Yanga na washambuliaji wa upinzani ambapo Jimmy Shoji aliuunga mpira ambao aliutema Kindoki dakika 38 na kuuzamisha nyavuni.
Mabadiliko aliyoyafanya kocha Mwinyi Zahera ya kumtoa Ibrahim Ajib na kumuingiza Amissi Tambwe yalileta uhai katika safu ya ushambuliaji Yanga.
Zahera pia, alimtoa Issa Mohamed na kumuingiza Juma Abdul ambaye alichukua majukumu ya Paul Godfrey ambaye alihamishwa na kucheza winga ya kulia ambako alikuwa anasaidia kupeleka mashambulizi mbele.
Zahera aliendelea kufanya mabadiliko dakika ya 74 alimtoa Haji Mwinyi na nafasi yake ilichukuliwa na Kelvin Yondani ambaye alikua anasaidiana majukumu na Andrew Vicent 'Dante' na Abdallah Shaibu 'Ninja' alipanda kucheza namba sita.
Yanga walipata faulo nje kidogo ya 18 baada ya mabeki wa Lipuli kumchezea rafu Tambwe, hata hivyo bahati haikuwa kwao baada ya Fei Toto kuipaisha.
Vikosi
Lipuli: Yusuph Mohamed, William Gallas, Paul Ngelema, Ally Sonso, Haruna Shamte, Fredy Tangalu, Miraji Athuman, Jimmyshoji Mwasondole, Paul Nonga, Daruwesh Saliboko na Zawadi Mauya.
Yanga: Klaus Kindoki, Paul Godfrey, Mwinyi Haji, Abdallah Shaibu 'Ninja', Andrew Vicent 'Dante', Faisal Salum 'Fei Toto', Mrisho Ngassa, Mohamed Issa, Heritier Makambo, Pappy Tshishimbi na Ibrahim Ajib.



0 Comments