

Pamoja na mshambuliaji Ibrahim Ajib kujiunga na TP Mazembe anategemewa kupata ushindani mkali wa namba kutoka kwa nyota kadhaa wa kikosi cha mabingwa hao wa DR Congo.Ajib ameripotiwa kujiunga na mabingwa mara tano wa Ligi ya Mabingwa Afrika, TP Mazembe kutokana na barua waliyowatumia Yanga na kuwataarifu kuwa wanamuhitaji nyota huyo msimu ujao.
Nahodha huyo wa Yanga anauwezo wa kucheza nafasi mbili uwanjani winga na mshambuliaji endapo atajiunga na klabu hiyo inayofundishwa na kocha Pamphile Mihayo Kazembe, anaweza kutumika katika maeneo mawili kama mshambuliaji au kiungo mshambuliaji anayecheza nyuma ya washambuliaji.
Endapo atatumika kama mshambuliaji atakutana na changamoto ya washambuliaji wawili wanaoaminiwa kwa sasa na kocha Mihayo mkongwe Tressor Mputu na Jackson Muleka.
Kama kocha Mihayo ataamua kumtumia Ajibu katika eneo la kiungo mshambuliaji, basi mkali huyo wa pasi za mwisho atakabiliana na changamoto ya viungo Elia Meschak, Rainford Kalaba na Abdoulaye Sissoko.
Ajib anatimka Yanga akiwa ameisaidia kushika nafasi ya pili kwenye msimamo huku akihusika katika mabao 24 ametoa pasi za mwisho 17 na amefunga mabao 7.



0 Comments