Windows

HATIMAYE CHELSEA WAKUBALI HAZARD KWENDA MADRID KWA BIL. 330/-



HUENDA shabiki wa Chelsea usiamini lakini ndiyo hivyo tena! Yale mazungumzo ya wiki mbili kati ya Eden Hazard na Real Madrid yamekamilika na muda wowote nyota huyo atasaini mkataba wa miaka minne.

Hata hivyo, Chelsea kukubali kumuuza staa huyo kumetajwa kuchangiwa na mmiliki wa klabu hiyo, Roman Abramovich, ambaye alisema ni bora apigwe bei kuliko kuondoka bure mwakani.

Gazeti la Sun limeripoti kuwa Real Madrid wamekubali kuuweka mezani mkwanja wa Pauni milioni 115 (zaidi ya Sh bil. 330 za Tanzania), kumpeleka Mbelgiji huyo kule Santiago Bernabeu.

Hazard alikuwa kwenye kiwango kizuri akiwa na uzi wa Chelsea msimu huu, akizitikisa nyavu za wapinzani mara 19 na kutoa ‘asisti’ 16 katika mechi 51 za mashindano mbalimbali.

“Tumekuwa tukijaribu kwa miaka mingi kumfanya Hazard awe mchezaji wa Real Madrid,” alisema Rais wa Madrid, Florentino Perez.

Chelsea watapewa Pauni milioni 100 na kisha wataongezewa Pauni milioni 15 hapo baadaye, ikielezwa kuwa mchezo wa jana dhidi ya Arsenal ulikuwa wa mwisho kwake akiwa na jezi za wakali hao wa jijini London.

“Navutiwa sana (Hazard) kuja Real Madrid na ni matumaini yangu kwamba anakuja mwaka huu. Ni mmoja kati ya wachezaji wakubwa,” aliongeza Perez.

Taarifa zimeongeza kuwa mkataba huo wa miaka minne utamfanya Hazard awe na uhakika wa kukinga mshahara mnono wa Pauni 400,000 (zaidi ya Sh bil. moja za Tanzania) kila wiki.

“Tulimtaka mwaka jana lakini mwaka huu ni rahisi zaidi kwa kuwa amebakiza mwaka mmoja tu katika mkataba wake,” alisisitiza rais huyo.

Kwa upande mwingine, inaaminika kuwa Blues walijipanga mapema kumpoteza Hazard na ndiyo maana walizama mfukoni na kutoa Pauni milioni 58 zilizotumika kumsajili Christian Pulisic.

Post a Comment

0 Comments