Pia dakika hizo zinatoa nafasi kwa Simba kufuta unyonge wa mwaka mmoja na miezi mitatu mbele ya Kagera ambapo haijapata ushindi dhidi ya timu hiyo kutoka mkoani Kagera.
Tangu Simba iliposhinda mabao 2-0 dhidi ya Kagera katika mchezo wa Ligi Kuu uliopigwa Uwanja wa Kaitaba huko Kagera, Januari 22 mwaka jana, imejikuta ikiwa mteja mbele ya vijana hao wanaonolewa na Kocha Mecky Maxime.
Mechi mbili zilizokutanisha timu hizo kwenye Ligi Kuu, Simba imejikuta ikichezea vichapo ikiwemo ile ya Mei 18, mwaka jana ambayo ilichapwa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Taifa mbele ya Rais John Magufuli. Ikumbukwe mchezo huo ulitumika kuikabidhi Simba ubingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita.
Kagera ilidhihirisha ubabe wao baada ya kuibuka na ushindi timu hizo zilipokutana tena Aprili 20, mwaka huu, Simba ilichapwa mabao 2-1 mjini Bukoba kwenye Uwanja wa Kaitaba.
Simba inaingia kwenye mechi ya leo ikiwa sawa kisaikolojia baada ya kupata ushindi katika mechi saba mfululizo kati ya hizo tano za ugenini, ikifunga mabao 18 na kuruhusu nyavu zao kutikiswa mara tano.
Kagera itakuwa na kibarua cha kufuta machungu iliyopata baada ya kupoteza mchezo uliopita nyumbani dhidi ya Mbao FC kwa mabao 2-1. Pia inapambana kujiondoa katika janga la kushuka daraja kwani licha ya kuwapo nafasi ya 12 kwa pointi 40, imezipiku timu mbili zinazoshika nafasi ya 19 na 18 kwa pointi tatu tu.
“Naridhika na kiwango cha timu yangu katika siku za hivi karibuni, kama mnavyoona imeimarika na inapata matokeo mazuri licha ya ratiba ngumu tunayokabiliana nayo.
Tunaingia kwenye mechi dhidi ya Kagera Sugar tukiwa na hesabu na malengo yaleyale ya kusaka pointi tatu ili tujiweke kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa,” alisema kocha wa Simba, Patrick Aussems.
Kocha wa Kagera, Mexime alisema timu iliyojiandaa vizuri kuelekea mchezo huo itapata matokeo.
“Siwezi kuwazungumzia Simba lakini kwa ufupi tumejipanga vizuri tumefika salama Dar na kila mchezaji ana ari nzuri hatuna majeruhi. Matarajio yetu ni ushindi tunajua mchezo hautakuwa rahisi lakini kutokana na maandalizi yetu dakika 90 zitaamua,” alisema Maxime.
Mjini Musoma, Yanga itakuwa ugenini kuvaana na Biashara United ikijaribu kuendeleza ndoto za kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu baada ya kutolewa katika Kombe la Azam Sports Federation kwa kulala mabao 2-0 dhidi ya Lipuli ya Iringa mwanzoni mwa wiki hii.
Endapo itafungwa leo mbele ya Biashara, ndoto ya Yanga kutwaa ubingwa zitazidi kufutika kwani itafanya Simba ihitaji kufikisha pointi 90 tu ili kutwaa ubingwa ambazo hazitaweza kufikiwa na Yanga.
“Kubwa tumejiandaa vizuri tunawaheshimu Yanga lakini mkakati wetu ni kushinda mchezo huo. Hatuko nafasi nzuri ndiyo maana tunapambana kushinda kila mchezo ili kujiweka pazuri, mashabiki waendelee kutusapoti ili kuibakiza timu kwenye ligi maana ndio malengo yetu,” alisema kocha wa Biashara United, Amri Said.
0 Comments