Mgunda alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya mpira kumalizika na timu yake kuchezea kichapo cha mabao 8-1 dhidi ya Simba kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, juzi.
Kocha huyo alisema kauli hiyo ilikuwa na maana mchezaji anapoingia uwanjani anapaswa kuwa na akili, utimamu wa mwili ili kutoa upinzani katika mechi husika.
Akizungumza kwa simu jana, mshambuliaji huyo wa zamani wa timu hiyo na Taifa Stars, alisema lawama za matokeo hayo anazibeba.
“Kocha yeyote duniani anayejua kusimamia taaluma yake, lazima ajue timu inafika muda gani sehemu ambako wanakwenda kucheza mechi, wachezaji wamekula chakula gani kwa siku hiyo, wanapumzika muda gani, yakifanyika hayo yote na timu ikafungwa basi hapo mwalimu na kikosi chake wataingia kwenye lawama.
“Kauli yangu ina hekima kubwa mwenye kuelewa ataelewa, nimetumia tafsida kwa maana hiyo wachezaji wangu sitaki kuwabebesha mzigo, naomba lawama zije kwangu licha ya kwamba kuna mambo yalikuwa nje ya uwezo wangu,” alisema Mgunda.
Kocha huyo alidai anaamini wachezaji wake walijituma, lakini walishindwa kupata pointi tatu kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo wengine walikuwa wamefunga Ramadhani.
Mgunda alirudia kauli yake akitaka wachezaji wasipewe lawama kwa kuwa ndani ya klabu hiyo kuna matatizo ambayo mashabiki hawawezi kufahamu na alitaka waachwe ili wamalize vyema mechi zilizobaki msimu huu.
“Tunacheza na Mtibwa Sugar Jumapili Uwanja wa Mkwakwani, nikianza kuyakuza haya basi nitaharibu kila kitu, bado wachezaji wangu wana safari ndefu, nimewapa pole na matokeo tunatakiwa kuendelea na maisha mengine,” alisema Mgunda.
Pia Mgunda alisema wachezaji wanacheza katika mazingira magumu ya kuvumilia, baada ya klabu hiyo kukumbwa na mtikisiko wa kiuchumi.
Wakati Mgunda akitoa kauli hiyo, Mwenyekiti wa Coastal ambaye pia Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi, Steven Mguto alisema timu hiyo iliwasili Dar es Salaam ikitokea Tanga saa chache kabla ya kuivaa Simba.
Mguto alisema umbali kutoka Tanga kwenda Dar es Salaam si wa kutisha na aliwataka wachezaji wasitoe sababu za kufungwa kwa kisingizio cha uchovu.
“Mnapofungwa basi maneno yanakuwa mengi kupita kiasi hasa tukicheza na hizi Simba na Yanga, ukweli ni kwamba timu ilifika siku ya mechi na sioni ajabu kwa hali halisi tulizonazo timu za mikoani, sasa inapokuja kuchanganywa matokeo mabaya tuliyopata nashindwa kuelewa.
“Wachezaji walipaswa kufanya kazi yao kwa bidii, mazingira hayo ni changamoto ambazo tumekuwa tukikumbana nazo mara kwa mara na si kuanza visingizio vya safari, kwangu sijaona kama ni sababu.
“Baada ya kufungwa idadi kubwa ya mabao tutakaa chini kwa pamoja na wachezaji wetu, naamini kila kitu kitakwenda sawa ila hatutakubaliana na matakwa ya kuona kwa namna yoyote ya kufungwa kwa sababu ya kufika Dar es Salaam siku ya mechi,”alisema kigogo huyo.
Hii ni mara ya pili Coastal kuchapwa idadi kubwa ya mabao, awali ilinyukwa 8-0 na Yanga 2015 licha ya kuweka kambi kwa siku kadhaa jijini.
0 Comments