KIPA namba moja wa timu ya Simba, Aishi Manula, amesema kwa namna alivyojizatiti hakuna mlinda mlango yeyote anayeweza kuchukua nafasi yake katika kikosi hicho.
Kauli hiyo ya Manula imekuja kutokana na kuwepo taarifa kwamba klabu ya Simba ina mpango ya kumsajili kipa wa Yanga, Beno Kakolanya, ili kuongeza ushindani katika nafasi hiyo.
Hivi sasa Manula anaonekana hana mpinzani katika kikosi hicho cha kocha Mbelgiji, PatrickAussems, licha ya uwepo wa Deogratius Munishi ‘Dida’ aliyesajiliwa msimu huu.
Akizungumza nasi , Manula alisema kama tetesi za mabosi wake kutaka kumsajili Kakolanya zitakuwa za kweli, ni jambo zuri kwa upande wake kwa sababu ataongeza idadi ya makipa watakaompa changamoto.
“Kupata namba moja kikosini si kazi rahisi lakini pia hata mwingine kukutoa si rahisi, nitafurahi kuona tunaocheza nafasi moja tupo wengi lakini wajue hakuna wa kuning’oa,” alisema Manula.
“Najiamini naweza kuisaidia Simba, inawezekana na mimi nina mapungufu yangu uwanjani lakini sioni wa kuchukua nafasi yangu labda kama nitakuwa na tatizo.
Aidha, Manula alieleza kuwa anafahamu majukumu yake ipasavyo na pia anajituma na kumshirikisha Mungu kwa kila anachotaka kufanya.
source : Bingwa
0 Comments