Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali nchini Marekani, Rod Rosenstein ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo akitarajia kuachia rasmi ngazi Mei 11 mwaka huu.
Rosenstein ambaye alikuwa mmoja wa waangalizi wa kazi iliyofanywa na tume maalum ya kuchunguza tuhuma za Urusi kuingilia uchaguzi wa Marekani, ameandika barua akimshukuru Rais Donald Trump kwa muda aliofanya naye kazi huku akigusia ucheshi wake.
“Ninakushukuru kwa nafasi uliyonipa ya kutumikia Taifa pamoja na ucheshi wako wakati wote tulipokuwa kwenye mazungumzo binafsi; na malengo uliyoweka wakati wa uzinduzi: uzalendo, umoja, usalama, elimu na maendeleo,” aliandika Rosenstein.
“Idara ya Sheria imeyafanyia kazi malengo hayo yote kwa kuzingatia utawala wa sheria. Utawala wa sheria ni msingi wa Marekani. Unalinda uhuru wetu, inaruhusu raia wetu kukua,” aliongeza.
Uhusiano kati ya Rod Rosenstein na Trump ulikuwa umeingia doa ambapo kuna wakati Rais huyo aliweka kwenye mtandoa wa twitter, Taswira inayomuonesha mwanasheria huyo akiwa amefungwa jela kwa uhaini.
Uamuzi wa mwanasheria huyo umekuja wakati ambapo William Barr anaendelea kuchukua nafasi yake mpya ya kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, hivyo Rosenstein anapaswa kushiriki katika makabidhiano ya majukumu ya ofisi hiyo.
Uamuzi wa Rosenstein umekuja siku chache baada ya tume iliyoongozwa na Robert Mueller kukamilisha uchunguzi na kutoa ripoti yao ambayo imeeleza kuwa haikuwa na ushahidi wa moja kwa moja kuwa timu ya Kampeni ya Trump ilishirikiana na Urusi kwenye uchaguzi wa mwaka 2016.
0 Comments