Windows

Man City yawika mbele ya Man United na kupanda kileleni

Manchester City ilirusha kombora kali katika harakati zao za kutwaa ubingwa wa pili mfululizo wa ligi ya Premier baada ya kupata ushindi rahisi wa derby dhidi ya watani wao wa mjini Manchester United uwanjani Old Trafford.

Vijana hao wa kocha Pep Guardiola walifahamu fika kwamba walistahili ushindi kwa vyovyote vile la sivyo Liverpool wangesalia kileleni mwa ligi na kuishikilia hatima yao wenyewe wakati zikisalia mechi tatu pekee ligi kukamilika.

City walijaribu kupenya katika ngome ya United kwa dakika 45 bila kufua dafu lakini wakaongeza giya katika kipindi cha pili na kupata pointi zote tatu zilizowaweka kileleni mwa ligi na mwanya wa pointi moja

Wacheza mechi sawa na Liverpool 35 kila mmoja. Bernado Silva alifunga bao la kwanza katika dakika ya 54 kabla ya Leroy Sane kugonga msumari wa mwisho kwenye jeneza.

Liverpool sasa lazima wajibu nyumbani dhidi ya Huddersfield Town ambao wameshushwa ngazi Ijumaa, wakati City watakuwa ugenini dhidi ya Burnely Jumapili.

Wolves 3 – 1 Arsenal

Arsenal walipoteza nafasi ya kutinga nafasi ya nne bora baada ya kufundishwa soka na Wolves dimbani Molineux. Ruben Neves aliwaweka wenyeji kifua mbele kupitia freekick kutoka umbali wa mita 25 kabla ya Matt Doherty kufunga bao la pili kwa kichwa. Diogo Jota aliongeza la tatu kabla ya kipindi cha kwanza kumalizika.

Beki wa Arsenal Sokratis alifunga bao la kichwa la kufutia machozi katika dakika ya 80. Ushindi huo unawasogeza Wolves kutoka nafasi ya kumi hadi ya saba, wakati Arsenal wanasalia katika nafasi ya tano, pointi moja nyuma ya nambari nne Chelsea na nne nyuma ya mahasimu wao wa kaskazini mwa London Tottenham.


Post a Comment

0 Comments