KUTOKANA na wachezaji nyota wa Simba Emanuel Okwi na Clatous Chama kukosekana kwenye mchezo dhidi ya Mbao uliochezwa Uwanja wa Jamhuri kumekuwa na tetesi kwamba wachezaji hao wamejiengua ndani ya kikosi hicho jambo ambalo uongozi wa Simba umepinga.
Ofisa Habari wa Simba Haji Manara amesema kuwa wachezaji wake wote muhimu ambao wamekuwa wakihusihwa kuondoka ndani ya kikosi hicho ambao ni Chama na Okwi hawachomoki kwa sasa.
Manara amesema kwa sasa wachezaji wote wa Simba wapo kambini Morogoro wakijiandaa na mchezo wao wa kesho dhidi ya JKT Tanzania utakaochezwa Uwanja wa Jamhuri.
"Wengi wanasema wanaongea kuhusu wachezaji wetu wa Simba, niwaambie wazi kwamba Okwi na Chama wote wapo kambini Morogoro kwa sasa, hivyo hakuna klabu itakayowachukua kwa sasa ni mali ya Simba," amesema Manara.
Baada ya Simba kumaliza mchezo wao dhidi ya JKT Tanzania watarejea Dar kujiandaa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa hatua ya robo fainali dhidi ya TP Mazembe.
0 Comments