BAADA ya Simba kupata kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya JS Saoura kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika ugenini nchini Algeria, sasa itakuwa ni vita dhidi ya Vita.
Simba ilifungwa mabao hayo mawili na kupoteza michezo yote mitatu ugenini msimu huu katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Tunajua kwamba unapopoteza ni lazima uwe umefanya makosa, hata hivyo msimamo wa kundi hilo la D unatoa matumaini kwa Simba kwamba inaweza kutinga robo fainali kama itaamua kufanya hivyo, na si kwa manenomaneno tu.
Msimamo unaonyesha kwamba JS Saoura inaongoza kundi ikiwa na pointi nane, ikifuatiwa na Al Ahly yenye pointi saba, sawa na timu inayoshika nafasi ya tatu, AS Vita ambayo nayo ina pointi saba, na Simba ghafla imeporomokea mkiani ikiwa na pointi sita.
Hata hivyo, Simba ina nafasi ya kusonga mbele kama itaitumia vizuri mechi yao inayofuata ya nyumbani, itakayochezwa Jumamosi ijayo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Simba inatakiwa ikusanye nguvu zote kwa ajili ya kuzitumia kwenye mchezo huu wa mwisho, maana sasa inahitaji ushindi tu wa aina yoyote ili kutinga robo fainali bila kuangalia matokeo mengine kati ya Al Ahly na JS Saoura, Waarabu watakaochinjana wenyewe.
Katika kundi hili, kumekuwa na maajabu kwelikweli, kila timu imeshinda nyumbani isipokuwa timu mbili tu za AS Vita iliyotoka sare ya 2-2 dhidi ya Al Ahly Congo, na JS Saoura iliyotoka 1-1 dhidi ya Al Ahly Algeria ndizo ambazo hazijafanikiwa kushinda nyumbani.
Hakuna timu yoyote hadi sasa kwenye kundi hili ambayo imeshinda ugenini, hali ambayo inaashiria ushindani wa juu kabisa katika mechi za mwisho, maana timu zitakazocheza nyumbani zinatarajiwa kushinda kama rekodi inavyoonyesha.
Lakini kwa Simba itakuwa na kazi kubwa sana. Tumewaona kwa mara nyingine AS Vita walipoichapa Al Ahly 1-0 juzi, hawa jamaa wanajua mpira na Simba wanapaswa kujua kwamba kweli wana vita dhidi ya Vita.
Ushauri wetu kwa Simba, kwa sasa wanatakiwa waifanyie kazi timu hii ya Vita, waichunguze vizuri kujua udhaifu wake, uimara wake na kujua pia mbinu ambayo wanaweza kuitumia kuwafunga.
0 Comments