JAMBO kubwa ambalo wamefanya wachezaji wa Simba linapaswa lipongezwe na kila mmoja kutokana na wawakilishi hao kupenya hatua ya robo fainali.
Haikuwa kazi rahisi ila wachezaji walijitambua na kujua majukumu yao na hatimaye ndoto ya wengi imekuwa kweli na sasa hatua kubwa ipo mikononi mwa Taifa na Afrika mashariki kiujumla.
Nikukumbushe kuwa wiki iliyopita tulipokutana hapa nilizungumzia juu ya nafasi ya Simba kimataifa kimahesabu na mwisho wa siku kila kitu kimekuwa sawa baada ya kushinda mbele ya wapinzani wao AS Vita.
Benchi la ufundi naamini lilitazama makosa ambayo waliyafanya hasa baada ya kucheza mechi nyingi za kimataifa hali iliyowapa uzoefu na kutambua mbinu mpya ambazo zimewafaa na kuwapa matokeo.
Pia wachezaji waliweza kujitambua na kuona thamani ya kuipeperusha Bendera ya taifa hasa kwenye michuano ya kimataifa jambo ambalo liliwapa morali na kupambana uwanjani mwanzo mwisho.
Niliweka wazi pia suala la kukata tamaa kuwa liwe mwiko kwa kila mchezaji hasa ukizingatia mchezo wenu wa mwisho mlikuwa nyumbani na hesabu zenu nyumbani ilikuwa ni kufa au kupona.
Mashabiki wa Simba na Taifa kwa jumla walionyesha upekee hasa kwa kujitokeza kwa wingi kwenye mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Taifa hali ambayo iliongeza nguvu kwa wachezaji kucheza kwa kujituma.
Pia ilikuwa ni raha kuona namna ambavyo Simba wanacheza kitimu huku mashabiki wakishangilia mwanzo mwisho hali hii inatakiwa iendelee kila siku na sio kwenye mechi za Simba na Yanga ndio mnajitokeza kwa wingi.
Yote kwa yote ushindi wa mabao 2-1 mliopata dhidi ya AS Vita isiwe mwanzo wa kubweteka na kuamini kwamba mnaweza kufanya mambo makubwa zaidi bila kuwa na nidhamu mtapotea kwenye ramani.
Pia Simba kwa kitendo cha kuuza siti zote mpaka za wana habari ambao walikuwa wakiwapa sapoti mwanzo mwisho isijirudie tena kwani mmewafanya wafanye kazi yao katika mazingira magumu.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jukumu lenu mlitimize kwa usawa na kufanya mambo kwa kufuata kanuni zinazotakiwa sio kujisahau katika mambo ambayo yanawahusu.
Jambo lingine kubwa kwa sasa ni kwa timu yetu ya Taifa, Taifa Stars ambayo itachezwa Machi 24, mwaka huu dhidi ya Uganda sasa kikubwa kinachotakiwa ni kujitoa kwa hali na mali kwa wachezaji pamoja na mashabiki hasa kwa kuipa sapoti timu yetu ya Taifa.
Uwezekano wa kufuzu Afcon kwa sasa upo mikononi mwenu wachezaji hivyo njia pekee ya kukata tiketi ya kufuzu Afcon ni ushindi wa mchezo wenu wa nyumbani ambao utakuwa ni mchezo wa mwisho na hakuna nafasi nyingine.
Hakuna haja ya kukata tamaa kutokana na namna ambayo mnakuwa kwenye mashindano haya ambayo nafasi hii ipo kwenu kuweza kufanya jambo la msingi na la heshima kwa Taifa ambalo linawategemea wawakilishi wetu wa timu ya Taifa.
Wakati ambao watanzania wanahitaji matokeo chanya ni huu wachezaji mna kazi kubwa kwa sasa ili kubeba furaha ya mashabiki wenu ambao wanapenda kuona namna ambavyo mnapata matokeo nyumbani.
Ushindi wenu ni ushindi wa Taifa kiujumla na ni wakati ambao watanzania wanahitaji kuona namna ambavyo wanabeba ushindi hasa nyumbani na mnapaswa mtambue kwamba timu ya Uganda ni ngumu hasa kwenye kupata matokeo.
Hivyo wachezaji msibweteke mna kazi ngumu ya kupata matokeo chanya kwa kuwa ugumu uliopo ni kutokana na namna ambavyo mnatakiwa kuwapa furaha mashabiki kwa kucheza kwa kujituma ndani ya Uwanja.
Mashabiki pia hapa mjitokeze kwa wingi kuona namna ambavyo mnawapa sapoti wachezaji wetu ambao wanaiwakilisha nchi yetu hasa kwenye hatua hii kubwa na inawezekana.
Kundi lenu L kwa sasa mambo yapo kawaida tu hasa ukitazama namna lilivyo, Lesotho watamenyana na Cape Verde huku Tanzania wakimenyana na Uganda hivyo kikubwa kinachotakiwa ni kuona namna ambavyo mnapenya.
Vinara wa kundi ni Uganda wenye pointi 13, Lesotho na Tanzania wana alama 5 huku Cape Verde wakiwa nazo nne, mechi za mwisho zitaamua nani apenye aungane na Uganda.
Kila la kheri tmu ya Taifa, benchi la ufundi lifanye kazi yake kuona namna gani watajipanga kuijenga timu na kuona ni namna gani inakuwa hasa kwenye upande wa matokeo chanya.
Kutoka Championi
0 Comments