Windows

Simba ijipange kweli, isiifanyie mzaha AS Vita



Mwishoni mwa wiki, wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba ilishindwa kutamba mbele ya JS Saoura baada ya kuwachapa mabao 2-0.


Simba iko Kundi D la michuano hiyo pamoja na Al Ahly ya Misri na AS Vita ya DR Congo.


Katika mchezo mwingine, timu hiyo ya DR Congo ililipa kisasi cha kufungwa mabao 2-0 na Al Ahly na yenyewe kuichapa bao 1-0 kwenye Uwanja wa Mashujaa mjini Kinshasa.


Huo ni mchezo wa pili wa timu hiyo kupoteza kwani mchezo wa kwanza ilifungwa na Simba kabla ya kulala kwa AS Vita.


Ilikuwa mchezo wa marudiano, kwani mechi za nyumbani na ugenini zinahusika zaidi katika michuano hii.


Matokeo hayo kwa ujumla yameitupa Simba mkiani mwa msimamo wa kundi hilo, kwani JS Saoura imefikisha pointi nane huku Al Ahly na AS Vita zikiwa na pointi saba kila mmoja wakati Simba ni ya mwisho ikiwa na pointi zake sita.


Mchezo wa mwisho kwa mujibu wa utaratibu, Simba itamalizia nyumbani na AS Vita iliyowafunga mabao 5-0 wakati Al Ahly itakuwa nyumbani kucheza na JS Saoura.


Kufanyika kwa michezo hiyo, kutakuwa na kumalizika kwa mechi za makundi yote kwani hata Shirikisho la Soka Afrika, CAF limepanga mechi zote zitaanza muda mmoja, kuanzia saa 1:00 usiku.


Simba iliyowasili jana kutoka Algeria ina kazi moja ya kuhakikisha inashinda mchezo huo.


Kibaya ambacho Simba itajiaminisha ni kama ilivyokuwa kwenye mechi ya Stella Abidjan katika Kombe la CAF mwaka 1993, ilipocheza fainali.


Simba iliingia fainali na katika mchezo wa kwanza ilikuwa ikihitaji bao 1-0 kutwaa ubingwa, lakini ikaja kufungwa kirahisi kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru). Ilitoka suluhu ugenini.


Matokeo hayo yalikuwa fadhaa kwa Simba lakini pia yalikuwa ya aibu mbele ya Rais wa Awamu ya Pili wakati huo, Ali Hassan Mwinyi.


Rais Mwinyi alimpa kombe la ubingwa nahodha wa Stellah na likavuka mpaka. Bahati hiyo haikuwahi kurudia tena. Simba ilishindwa kujipanga katika mchezo ule kiasi cha kufungwa kwa kuwa walijiamini kupita kiasi kwamba tayari wameshinda mchezo huo ilhali mambo yalikuwa siyo.


Kinachotakiwa sasa, baada ya kufika jana, ni kuanza mikakati ya dhati, kuhakikisha AS Vita anakufa mapema kabisa.


Kama ilivyo kwenye kundi hilo, timu nyingi zimeshinda mechi zao za nyumbani, ndivyo inatakiwa kuwa, lazima Simba kumaliza kwa ushindi.


Lakini watashinda vipi, ni wachezaji kujituma na wana kila sababu ya kufanya hivyo.


Wachezaji wanatakiwa wafahamu kuwa uwanja wa nyumbani haufanyiwi makosa siku zote, kwa kuwa timu zinacheza mbele ya mashabiki wao wakipewa nguvu ya ushindi. Simba tayari imeshautumia vyema uwanja wa nyumbani kwa kuzifunga JS Saoura lakini pia na Al Ahly katika mfululizo wa michuano hiyo mikubwa ngazi ya klabu Afrika.


Pamoja na ushindi wa mechi hizo, Simba wana nafasi ya kushinda kwa kuwa wachezaji watakuwa katika hali ya hewa iliyozoeleka na mazingira yaliyozoeleka, ndiyo maana timu nyingi hutumia vema uwanja wa nyumbani hasa timu za Kundi D matokeo yalivyokuwa.


Itashangaza, pamoja na kwamba ni mchezo unaweza kuzalisha matokeo ya aina yoyote, lakini kufungwa katika mchezo huo, itafifisha matumaini ya mashabiki na kila mmoja mpenda soka kuona Simba inatinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.


Cha msingi ni kwa benchi la ufundi la Simba, kukaa pamoja na wachezaji, kuwajenga kisaikolojia, watambue umuhimu wa kushinda mchezo huo na zaidi kucheza kwa nidhamu ili kuepuka kadi zisizo za lazima ambazo baadaye hugharimu timu.


Ni dhahiri kuwa wachezaji wakifanya mazoezi ya maana katika siku mbili kurudi mchezoni baada ya kichapo cha Algeria, wakijengwa kisaikolojia, ushindi wa mabao utapatikana na kuiwezesha Simba kuivusha Tanzania kuingia katika historia mpya, safari hii katika hatua ya Nane Bora Afrika.


Hakuna kinachoshindikana, kama jitihada, nguvu, kazi na juhudi binafsi kwa wachezaji uwanjani, wanaweza kufika mbali. Simba imeshapata somo la kutosha ilipopambana na JS Saoura lakini pia na Al Ahly na tunaamini kwa AS Vita hakuna kinachoshindikana.


Tunawatakia maandalizi mema wachezaji na viongozi pamoja na benchi la ufundi, kuhakikisha wachezaji wanapata mahitaji yao muhimu na kuwatia moyo ikiwemo kuwajenga kisaikolojia wafanye vizuri katika mechi hiyo muhimu.


Ushindi wa Simba hautabaki kwa Simba, ushindi wa timu hiyo utakuwa wa Watanzania wote na sifa itabaki kwa Watanzania wote kwa kuwa timu ni ya Tanzania.


Kingine ambacho tunakiona ni kwa mashabiki wa soka bila kujali itikadi, kuibeba Simba kwenye michuano hiyo.


Tunasema kuibeba kwa maana ya kwamba kuwashangilia na kuwapa moyo.


Kufanya vizuri kwa Simba ikiingia robo fainali hadi nusu fainali, kutakuwa na faida kwa timu za Tanzania kuongezeka.


Kwa mujibu wa utaratibu wa CAF, timu itakayoingia nusu fainali, ina nafasi ya kuja na timu nyingine kwa nafasi yake.


Sasa kama kuna faida hiyo, kwanini Simba iachwe yenyewe? Ipewe nguvu ili timu zaidi iingie Afrika kwa nguvu za kila mmoja.


Post a Comment

0 Comments