

NA SALEH ALLY
MECHI kati ya Yanga dhidi ya Alliance iliyochezwa juzi Jumamosi, imekuwa na malalamiko mengi na makubwa. Lawama inatokea katika kila upande.
Yanga wana imani kwamba walicheza vizuri na kuibuka na ushindi, lakini Alliance wamekuwa wakilalama kuhusiana na bao walilofungwa huku wakisisitiza kwamba haikuwa sahihi maana hata wao walifunga na bao likakataliwa.
Yanga wameibuka na ushindi wa bao 1-0 na kuendelea kujikita kileleni mwa Ligi Kuu Bara, hii inawafanya waendelee kuwa mbele wakipambana kuhakikisha wanakuwa mabingwa.
Kwao Yanga ni jambo zuri sana kwa kuwa lengo kuu ni kuwa mabingwa wa Ligi Kuu Bara dhidi ya watani wao Simba ambao wana rundo la viporo.
Msingi wa lawama katika mechi hiyo ni jambo la kuangalia kwa macho mawili. Nasema hivyo kwa kuwa tunaweza kujifunza mengi na kutakuwa na usahihi jambo hili likiangaliwa bila ya ushabiki.
Kwamba mwamuzi alikuwa ni mtoa haki sahihi? Nina bahati mbaya moja kwamba mechi hii niliiangalia kwa vipande mtandaoni kwa kuwa sipo nyumbani Tanzania.
Pamoja na hivyo, nimegundua mambo mengi sana ambayo nimejifunza lakini ningependa kuachana na lawama za kazi ya mwamuzi ilivyokuwa na badala yake nijikite katika suala la nidhamu.
Nisisitize, kama mwamuzi hakuwa sahihi basi tuangalie kwa jicho lisilo na ushabiki na baada ya hapo hatua zichukuliwe.
Wakati hatua zinachukuliwa, lazima tuwe tumejiridhisha kuwa kweli kosa lilifanyika na si kuangalia kwa matakwa ya kishabiki maana utani wa Simba na Yanga umegeuka kuwa kama vita, jambo ambalo si sahihi.
Nimeona matukio kadhaa ya wachezaji wa Alliance, hakika si sahihi. Mfano mchezaji mmoja aliyempapasa mchezaji wa Yanga makalio lakini yule aliyemkita mchezaji wa Yanga teke la tumboni na mengine ya namna hiyo ya utovu wa nidhamu unaoonyesha malezi mabovu.
Mimi nimecheza mpira wa uswahilini ambao mchezaji anaweza kuchagua aina yake ya kuwa kwa maana ya kufanya anavyotaka yeye kwa kuwa hakuna malezi ya kisoka.
Vipi leo timu kama Alliance ambayo navutiwa nayo kwa aina ya kiuchezaji kwa kuwa inaonekana soka lao ni la mafunzo.
Nashangazwa zaidi na kuona wao Alliance wanafanya utovu wa nidhamu ambao kamwe hauwezi kufanywa na timu ambayo ina maendeleo ya mafunzo kiuchezaji.
Alliance wamekuzwa katika misingi ya kisoka, hata kama watakuwa na wachezaji wengine wageni ambao wameingia wakijiunga na timu yao bado hawawezi kubadili tabia ya ubora wa kikosi kizima.
Vipi mchezaji kutoka Alliance anaingia katika makundi ya upapasaji makalio ya wachezaji wengine tena katika sehemu ambayo haina purukushani yoyote?
Kwa nini tusione wachezaji wa Alliance wakiwa gumzo la mfano kwa kuwa timu yao imekuwa na malezi sahihi tena ya muda mrefu na wengi wao wamelelewa kama vijana wadogo hadi kufikia hapo walipo.
Huenda Alliance wangeweza kuwa mfano na mwanzo wa mabadiliko la soka ya Tanzania na si kuingia kwenye kundi la kufanya mambo kwa kubabaisha kama ambavyo imeanza kuonekana.
Ushauri wangu kwa uongozi wa Alliance unapaswa kukemea hili kwa wachezaji wake badala ya kukubali liendelee kwa kigezo Yanga ilipendelewa.
Hili halihusiana na Yanga kupendelewa na si jambo jema kwa afya ya soka ya Alliance ambayo ina vijana wengi wanaendelea kukua na hawapaswi kuona upuuzi wa namna hii usiovumilika.
Uongozi wa Alliance lifanyieni kazi hili, limalizeni na kuifanya Alliance iendelee kuwa na afya sahihi ya mapambano muendelezo.



0 Comments