Bingwa wa michezo ya Olimpiki ya Beijing 2008 na bingwa mara tatu wa mbio za mita1,500 Mkenya Asbel Kiprop anatumai kuwa hatimaye jinamizi linalomuandama litawekewa kikomo wakati Kitengo cha Uadilifu katika Riadha – AIU kitakapofanya uamuzi wa mwisho kwenye kesi ambayo iliushangaza mchezo huo.
Akizungumza kabla ya kuondoka Nairobi Jumatano kwenda London ambako uamuzi huo utatolewa, Kiprop kwa mara nyingine alisisitiza kuwa hana hatia baada ya AIU kuthibitisha mwezi Mei mwaka jana kuwa matokeo ya vipimo vyake vya nje ya mashindano vilivyofanywa nyumbani kwake Iten mnamo Novemba 7, 2017 vilitoa matokeo yaliyoonyesha kuwa alitumia dawa zilizopigwa marufuku za kuongeza nguvu kwenye damu za EPO.
Vikao vitatu vya kusikilizwa kesi yake vilivyopangwa Septemba na Novemba mwaka jana na kingine Januari mwaka huu, vilisogezwa Machi 21, na kumuacha mwanariadha huyo ambaye alishinda dhahabu katika mbio za wanaume za mita 1,500 mjini Daegu 2011, Moscow 2013 na Beijing 2015 kwenye mashindano ya dunia ya IAAF katika hali ya sintofahamu kitaalum.
Hata hivyo, AIU ilimruhusu Kiprop kuanza kufanya mazoezi ya kibinafsi mwezi Novemba lakini bado ikamzuia kushiriki katika mashindano yoyote ya ushindani.
“Nnaomba ukweli ujulikane na bila kucheleweshwa. Kesi hii imenigharimu sana kifedha, kihisia na pia kunizuia kufanya mchezo nnaoupenda zaidi. Umekuwa wakati mgumu kwangu na natumai kuwa uamuzi huu hautacheleweshwa tena,” Amesema Kiprop kabla ya kuelekea London akiandamana na wakili wake Katwa Kigen.
0 Comments