WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, ametoa wito kuwa mbinu za Simba zilizotumika kuwafunga SC Vita kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar, hasa katika uhamasishaji wa mashabiki kuendelea kutumika katika mchezo wa timu ya taifa, Taifa Stars dhidi ya Uganda.
Taifa Stars inatarajia kuikaribisha Uganda, keshokutwa Jumapili katika mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zinazotarajiwa kufanyika nchini Misri, mwaka huu.
Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani wa hali ya juu kutokana na wapinzani wa Stars, Uganda kuwa tayari wamefuzu lakini wakihitaji kuweka rekodi ya kutokufungwa katika hatua za makundi.
Mwakyembe alisema kuwa ni lazima Taifa Stars ipambane na kuweza kuifunga Uganda ili kushiriki Afcon.
“Ni lazima tuwafunge Uganda sababu ni timu ya kawaida na cha msingi ni wachezaji wetu kuwa makini uwanjani na mashabiki wajitokeze kwa wingi kama ilivyokuwa kwenye mchezo wa Simba.
“Ni zamu yetu kwenda Misri, Watanzania tuungane kwa pamoja kuweza kujitokeza kwa wingi ili kuisapoti Taifa Stars,” alisema Mwakyembe.
Katika hatua nyingine, Waziri Mwakyembe amempongeza msanii wa Bongo Fleva, Rayvanny kwa kuandaa wimbo maalum wa kuisapoti Taifa Stars na kumtaka Jumapili awepo uwanjani.
0 Comments