Uongozi wa Yanga umeanza maandalizi ya mikakati yenye lengo la kuisogeza timu hiyo karibu zaidi na wadau wake katika kuelekea msimu ujao.

Hiyo, ikiwa ni siku chache tangu timu hiyo iunde kamati yake mpya ya uhamasishaji wa kuchangia fedha katika klabu hiyo inayoongozwa na mwenyekiti wake, Anthony Mavunde ambaye ni Naibu Waziri Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu, pia ni Mbunge wa Dodoma Mjini.

Kamati hiyo, tayari imeanza kazi yake na kuweka malengo ya kukusanya shilingi bilioni 1.5 kutoka kwenye matawi ya kila mkoa ili kufanikisha usajili wa wa msimu ujao.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani kamati imepanga kukitangaza kikosi chao kipya kabla ya kuanza msimu mpya utakaoendana na mauzo ya jezi, bendera, skafu na vitu vingine kwa kutumia nembo ya klabu hiyo.

Mtoa taarifa huyo alisema, kocha wa timu hiyo tayari ameanza mipango yake ya kuwaongezea mikataba mipya wachezaji wake ambao mikataba yao inamalizika kwa kuwapa mipya kabla msimu haujamalizika.

 Aliongeza kuwa, kocha huyo tayari ametoa mapendekezo ya usajili wa wachezaji wapya aliowapendekeza wa kimataifa kutoka nchi za Mali na Ghana.

“Uongozi wa Yanga unakusudia kuanzisha utaratibu wa kukaribisha msimu mpya kwa kuwakutanisha Wanayanga katika tukio ambalo pia litatumika kutambulisha wachezaji wapya, jezi na bidhaa nyingine za klabu.

“Utaratibu huo umekuwa ukifanyika na Simba kwa misimu iliyopita, hiyo ni baada ya kupitia ushauri na mapendekezo yaliyotolewa na kamati hiyo mpya ya uhamasishaji wa uchangiaji wa fedha.

“Utaratibu huo tumepanga kuanza nao mwaka huu tukielekea mwishoni mwa msimu na kikubwa tunataka kuwashirikisha wadau na mashabiki wa Yanga ili kufanikisha malengo yetu,” alisema mtoa taarifa huyo.

Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Dismas Ten alithibitisha hilo kwa kusema: “Ni kweli Yanga hivi sasa ipo kwenye mipango mikubwa ya kuhakikisha tunatoka hapa tulipo na kwenda mbele, hivyo kuna mambo mengi yanakuja.”