KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema kuwa kwa sasa hesabu zake ni kuona anapata matokeo chanya kwenye mechi zake zote zilizobaki ili kubeba ubingwa wa Ligi Kuu pamoja na kombe la Shirikisho kutokana na aina ya wachezaji alionao.
Zahera amesema kuwa licha ya ugumu ambao wanapitia kwa sasa anaamini wachezaji wake ndio watafanikisha suala la kubeba mataji kwenye mashindano ambayo wanashiriki hivyo ni suala la muda tu kupata matokeo.
"Ajibu (Ibrahim) akiwa kwenye ubora wake na Makambo (Heritier) akiwa kwenye ubora basi hawa wakiwa ndani ya uwanja sina mashaka na suala la kupata matokeo najua ni suala la muda tu.
"Tambwe (Amiss) yeye anafanya vizuri akitokea benchi kwa kuwa amepindua matokeo mara nyingi na ninamuamini, wachezaji wote wanacheza wakiwa ni timu pia wengine wapo timu ya taifa kama Kelvin Yondani, Feisal Salum, Andrew Vincent na Gadiel Michael, naona tukifanya vizuri licha ya kupitia kipindi kigumu.
"Kwa kila mchezaji ndani ya Yanga anatambua thamani ya jezi ya Yanga na anaheshimu timu yake hivyo malengo yetu yatatimia," amesema Zahera.
Yanga ipo nafasi ya kwanza kwenye msimamo baada ya kucheza michezo 28 ikiwa na pointi 67.
0 Comments