Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Löw ameangusha bomu! Ametangaza kuwa washindi wa Kombe la Dunia 2014 Thomas Müller, Jerome Boateng na Mats Hummels hawako kwenye mipango yake ya usoni.
Löw aliwaambia wachezaji hao watatu wa Bayern Munich kabla ya kukitaja kikosi cha mchezo wa kirafiki dhidi ya Serbia mjini Wolfsburg katika wiki tatu zijazo na mchuano wa kufuzu katika Euro 2020 dhidi ya Uholanzi mjini Amsterdam mnamo Machi 24.
Kati yao wote, Hummels na Boateng wana umri wa miaka 30, na Müller bado ana umri wa miaka 29 pekee, wamecheza mechi 246 kwa timu ya taifa ya Ujerumani na walikuwa kitovu cha timu ambayo ilishinda Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil.
Hata hivyo, majanga yam waka jana katika Kombe la Dunia nchini Urusi yaliifanya Ujerumani kutupwa nje katika hatua ya makundi kutokana na mchezo wa kiwango cha chini mno kutoka kwa nyota wa Löew wakiwemo hao watatu.
“2019 ndio mwaka wa mwanzo mpya wa timu ya taifa ya kandanda ya Ujerumani,”Alisema Löw.
“Ilikuwa muhimu kwangu binafsi kufafanua mawazo yangu na mipango yangu kwa wachezaji na mameneja wa FC Bayern.” Aliongeza Löw aliyesafiri hadi Munich kzungumza na wachezaji hao watatu.
Kocha huyo mwenye umri wa miaka 59, ambaye aliiongoza Ujerumani kubeba Kombe la Dunia nchini Brazil, aliwashukuru “Mats, Jerome na Thomas kwa miaka mingi yenye mafanikio makubwa sana wakiwa pamoja.”
0 Comments