Windows

Harambee Stars yapata mdhamini mpya

Timu ya taifa ya kandanda ya Kenya – Harambee Stars imepata mdhamini mpya. Kampuni ya kubashiri matokeo ya mechi ya Betin imezinduliwa leo rasmi katika hafla iliyoandaliwa jijini Nairobi.

Kampuni hiyo imewekeza kitita cha shilingi milioni 20 kwa mkataba wa udhamini wa mwaka mmoja, ambapo shilingi nyingine milioni 5 zitatumika katika kushughulikia sare za timu. Harambee Stars tayari wamefuzu katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika 2019 ambazo zitaandaliwa kuanzia Juni 21 hadi Julai 2 nchini Misri, kumaanisha kuwa fedha za Betin zitakuwa na msaada mkubwa sana katika kuipiga jeki timu ya taifa amabayo inarejea katika dimba hilo kubwa la Afrika baada ya kuwa pembeni kwa miaka 15.

Rais wa chama cha mpira Kenya – FKF Nick Mwendwa amesema ufadhili huo mpya utakuwa na mchango mkubwa kabisa katika kupata mafanikio kwenye mashindano ya AFCON.

“..tayari tumekubaliana kuwa katika kila ushindi watakaopata Misri, tutawapa shilingi milioni 7 za Kikenya na kama watashinda dimba hilo, wachezaji watapewa hadi shilingi milioni 120, na hiyo ni ukiondoa fedha za waandalizi.”

Mwenda amethibitisha kuwa serikali imeahidi kuipa Stars kitita cha shilingi milioni 240 kwa ajili ya kinyang’anyiro cha AFCON. Mkurugenzi wa Mauzo wa Betin Kenya Carlo Buttaci amesema watafanya kila wawezalo kuisaidia Stars nchini Misri na pia watakisaidia chama cha mpira Kenya katika kukuza vipaji vya chipukizi mashinani.


Post a Comment

0 Comments