

LEO Uwanja wa Kaitaba, majira ya saa 10:00 jioni vumbi litatimka kati ya Kagera Sugar na Azam FC, mkoani Kagera, kwenye mchezo wa kombe la Shirikisho hatua ya robo fainali.
Azam FC wamepania kuonyesha ubabe mbele ya wapinzani wao ili kutinga hatua ya nusu fainali katika mchezo wa leo.
Ofisa Habari wa Azam FC, Jaffary Maganga amesema wanatambua ushindani uliopo na namna wapinzani walivyo ila hakuna namna watapambana.
"Tumejipanga kisawasawa, tupo kamili na tupo tayari licha ya changamoto ya hali ya hewa hapa Kagera hilo halitupi taabu tunahitaji matokeo ili kusonga mbele," amesema Maganga.
Kocha wa Kagera Sugar, Mecky Maxime amesema hawana hofu amewapanga wachezaji wake kutafuta matokeo chanya.
"Tumejiandaa na tupo tayari kwa ajili ya mchezo wa leo hakuna haja ya kuwa na hofu kikosi chetu kipo sawa na tutaonyesha ushindani," amesema Maxime.
Kagera Sugar na Azam FC atakayeibuka kidedea atakutana na mbabe wao KMC ambaye tayari ameshapenya hatua ya robo fainali na kutinga nusu fainali baada ya kuibuka na ushindi mbele ya African Lyon.




0 Comments