Windows

TSHISHIMBI AMESHAJUA NI MKAZI WA DAR ES SALAAM NA ANAISHI NA KINA NANI!




Na Saleh Ally
UNAJUA kiungo Papy Tshishimbi raia wa DR Congo amerejea na kuwa gumzo kwa mara nyingine.


Mashabiki wa soka, sasa wameanza kuzungumza kuhusiana na yeye kwamba amerejea katika kiwango kinachotakiwa kuliko wakati wa takribani miezi minne hivi, mambo yalikuwa ilimradi.


Wakati akitoka Mbabane Swallows na kujiunga Yanga kiwango chake kilikuwa cha juu na alionyesha kuwa ana nia ya kufanya makubwa.


Katika mechi takribani 15 za mwanzoni, Tshishimbi alionyesha uwezo ambao ungekuwa ni mfano wa kuigwa na Yanga hawakuwa na sababu ya kujiulaumu kumpata.

Maana alikuwa na mambo hivi ambayo mchezaji bora angetakiwa kuwa nayo hasa katika nafasi ya kiungo ambayo anacheza.

Kwanza ni uwezo wa kukaba, pili kuchezesha timu, tatu kuwa kiongozi pale mambo yanapochafuka kwa maana ya kuibeba timu na kubadilisha na mwisho ni uhamasishaji pale wanapofungwa bao na kadhalika.


Tshishimbi alikuwa akionyesha ni mchezaji asiyeogopa, mchezaji ambaye yuko tayari kwa mapambano ya aina zote bila ya kujali anakutana dhidi ya mchezaji au timu ipi.



Kadiri siku zinavyosonga tuliona akizidi kuporomoka, umaarufu wake ukapungua na baadaye akaanza kupoteza "nuru" katika kikosi hadi alipokaa nje.

Uzuri wakati anakaa nje alikuwa na kisingizio cha majeraha. Lakini hata baada ya kurejea, hakuwa na nafasi ya kufanya vizuri kwa wakati mwingine kama ilivyokuwa awali.


Kawaida anayetokea katika hali ya umajeruhi, hurejea taratibu. Lakini unaona kwa Tshishimbi ilishindikana na kukawa na ugumu kidogo kwake.


Inaweza ikawa vigumu sana kumueleza ukweli kwa kuwa wako wanaoweza kuamini anasakamwa lakini yeye anaweza kufikiria hivyo.


Ukweli suala la kuporomoka kiwango kwa wachezaji wengi na hasa wa kigeni au wageni wa Jiji la Dar es Salaam wanaweza kuwa shahidi wa hilo kwamba, unapoingia katika jiji hili mambo ni tofauti.


Pale bendi za muziki wa dansi zikianza kukuimba wakitanguliza jina la "Papaa" inabidi ujihadhari mapema kwa kuwa umaarufu wako unakuwa kwa upande wa pili na usipokuwa makini unaweza kukuangusha.


Watanzania hasa wanaoishi Dar es Salaam wana starehe nyingi, mojawapo ni ukarimu na kama unapenda starehe kama wanakukubali basi zinaweza kukumaliza na kukupotezea kabisa ile hali ya umakini katika kile unachokifanya.


Mfano, wakupeleke kila ukumbi usiku wa kuamkia Jumamosi. Utarudi nyumbani kwako saa 10 alfajiri na saa 12 unatakiwa mazoezini. Huu ni mfano wa mwanasoka, unafikiri ataweza kuwa katika kiwango chake!


Watu hao wengi ni maarufu, waungwana na wanaopenda watu wanaowapenda wao kufurahi na kula raha ya maisha na wakati mwingine wangependa wao kuonekana wako karibu na mtu maarufu, hivyo kukuunganisha na watu wa starehe wakiwamo wanawake mbalimbali, wala haliwezi kuwa jambo la ajabu na ukitaka kubadilisha kwa kila aina, hakutakuwa na shida.


Yote haya sina maana Tshishimbi ndiye amefanya, lakini najaribu kukumbusha kuhusiana na wapenda mpira wanapokuwa katika taswira ya upande wa pili kuhisiana na starehe.

Kurejea kwa Tshishimbi, maana yake amejiongeza na kukumbuka kwa mara nyingine kilichomleta Tanzania kuwa ni kazi na si "mapokeo ya uungwana".


Ninaamini kuna sehemu alipokuwa anakosea na ameamua kuparekebisha ili kuhakikisha anarejea katika kiwango kilichowavuta Yanga na kuamua kumhamishia Tanzania kwa ajili ya kufanya nao kazi.


Kwa upande mwingine kurejea kwa Tshishimbi katika kiwango bora kunaonyesha Kocha Mwinyi Zahera ni mtu anayependa haki kwa kuwa wakati kiwango chake kimedorora, licha ya kuwa raia wa DR Congo kama yeye, bado alimtupa nje kwa kuwa kwake "Ni Kazi Tu".


Sasa amerejea, amempa nafasi na ameonyesha kweli anastahili kucheza. Hili liwe funzo kwetu kwa kuwa inaonekana tayari Tshishimbi mwenyewe amejifunza na sasa anachotaka ni kuyatumia mafunzo hayo kufanya vema.


Karibu tena Tshishimbi tuendelee kujifunza kupitia soka. Kitu kizuri kwako ni tayari umejua unaoishi nao ni watu wa namna ipi!




Post a Comment

0 Comments