Windows

NGOMA, CHIRWA CHANZO CHA KUFUKUZWA PLUIJM, MWAMBUSI







NA SALEH ALLY
TUMEELEZWA taarifa ya kutupiwa virago kwa makocha Hans van Der Pluijm na Juma Mwambusi katika Klabu ya Azam. Awali ilikuwa ni kama tetesi, lakini baadaye mtandao wa klabu hiyo ukathibitisha.

Azam FC imeonekana kutokuwa na mwendo mzuri licha ya kwamba iko katika nafasi ya pili katika Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 50 baada ya kucheza mechi 25.

Wastani wa Azam kwa mchezo ni kukusanya pointi mbili ikiwa na maana ya sare na ushindi ni sawa ikiwa kitakwimu kwa maana ya msimamo unaonyesha Azam imeshinda mechi 14, sare 8 na imepoteza 3.

Kwa maana ya mwendo wa kawaida, unaweza kusema timu hiyo haijafanya vizuri sana lakini kwa kile ambacho wanachokitaka wamiliki wa timu hiyo kinakuwa hakijatimia na jibu mwisho linakuwa ni kufeli.

Kikosi cha Azam kinafungwa na suala la ufungaji wa mabao, hilo ndilo tatizo kubwa sana hasa kama utaangalia msimamo. Mfano, Yanga wanaoongoza, baada ya mechi 25 wamefunga mabao 42 wakati Azam wamefunga mabao 33.

Simba ambao wamecheza mechi 18, wao wamefunga mabao 38 ikiwa zaidi ya mabao matano dhidi ya Azam FC licha ya kwamba wana mechi pungufu saba dhidi ya Azam FC. Katika hali ya kawaida unaweza kufikiria Simba watafunga mengine mangapi katika kila mechi kati ya hizo saba.

Kama watakuwa na wastani wa bao moja tu katika kila mechi, maana yake tofauti ya ufungaji wa mabao itakuwa ni 12 dhidi ya Azam FC ambao ina fowadi ya mamilioni ya fedha!

Azam FC imeangushwa kwa kiasi kikubwa na utendaji duni wa washambulizi wake ambao Pluijm aliamini watakuwa msaada mkubwa bila ya kuangalia vizuri alichokuwa akikifanya.

Wakati anajiunga na timu hiyo, Pluijm alikuwa amepata mafanikio makubwa kabla akiwa na Yanga. Baada ya kwenda Singida United alifanikiwa kuifikisha fainali ya Kombe la FA ingawa ilipoteza mchezo huo dhidi ya Mtibwa Sugar.

Bado mafanikio yake ya Yanga yaliendelea kuwa kumbukumbu ambayo binafsi naona ndio imemponza kwa kiasi kikubwa kwa kuwa unaona imsogeze shimoni kwa kuwa wachezaji aliowaamini ndio chanzo cha yeye kufeli.

Donald Ngoma aliyekuwa naye Yanga na baadaye akamuongeza Obrey Chirwa raia wa Zambia ambaye pia alifanya naye kazi Jangwani. Unaweza kusema wamejitahidi na hasa Chirwa lakini bado hawajawa na kile kiwango kinachoweza kuwafanya waitwe washambulizi hatari.

Ngoma si yule tena na sote tunajua aliondoka Yanga akiwa tayari amepotea kabisa. Kisingizio kilikuwa majeruhi na Azam FC wakakubali kumsajili akiwa mgonjwa na kuchukua uamuzi wa kumtibu.

Si jambo baya lakini Ngoma ameshindwa kuonyesha kile kilichotegemewa na wengi na kama ni katika mfumo wa Pluijm lazima alikuwa afanye vizuri kwa kuwa ni kitu ambacho tayari amekuwa akikitumikia kwa muda mrefu.

Wakati Pluijm alipopata nafasi ya kuinoa Azam FC alikuwa na kila sababu ya kuhakikisha anapata mfungaji bora kabisa ambaye ana uwezo wa kuwa tishio katika kikosi chake.

Pluijm ni kocha ambaye amefundisha nchini Ghana na analijua soka la Bara la Afrika kwa upana. Kusingekuwa na ugumu kwake kupata mshambulizi bora na wa kiwango cha juu zaidi ya Ngoma na Chirwa.

Azam FC wanaweza kuonekana hawako sawasawa kama kweli wamepitisha uamuzi wa kuachana na Pluijm. Lakini tunaweza tusijue kuhusiana na kiwango walichokitumia katika usajili wa wachezaji hao na vipi Pluijm aliwahakikishia kitakachofuatia.

Ngoma na Chirwa ni wazoefu wa Ligi Kuu Bara, hakuna ubishi walikuwa na kila sababu ya kufanya vema katika ufungaji na si idadi ya mabao matano kwa Ngoma na moja kwa Chirwa waliyo nayo kwa sasa.

Ukiangalia katika msimamo wa wafungaji, hakuna mchezaji yeyote kutokea Azam FC ambaye anapambana kuwania kiatu cha mfungaji bora wa ligi hiyo. Maana yake hakuna mshambulizi hatari anayetisha katika kikosi cha Azam FC hadi sasa ligi imekwenda mzunguko wa pili.

Vipi timu inayowania ubingwa isiwe na mshambulizi hatari ambaye mbio zake za ufungaji zinaonekana kuwa ni tishio kwa mabeki wa timu nyingine. Vipi hakuna kiungo anayeogopewa au gumzo kwa sasa katika kikosi hicho?

Hesabu za Pluijm hazikuwa nzuri na hakutaka kufikiria zaidi kwa sababu aliijua staili ya Azam FC kwamba ni timu ambayo hawasubiri wanapoona kuna dalili za kufeli.


Post a Comment

0 Comments