

Na Saleh Ally
WANADAMU tumekuwa na tabia ya kutokuwa tayari kukikubali kitu tulichonacho mkononi kwa wakati husika sababu tunaamini hakina ubora.
Badala yake tumekuwa na tabia ya kukikubali hichohicho wakati kinapokuwa hakipo mikononi mwetu.
Wakati kipo mkononi mwako unaweza kuwa na rundo la sababu ukiamini kitu hicho hakina maana kwako hata kidogo. Ukaanza kuona kitu hicho kina mambo mengi ambayo si sahihi.
Ukakikosoa na kuona ubora wake hauko sawa kwa kutoa sababu nyingi sana. Lakini siku hakipo, unaweza kugeuza kuwa mfano wa simulizi wa ubora wake.
Hii imekuwa ni tabia yenye mwendelezo katika jamii yetu na mwendelezo wake unaendelea katika maisha ya kawaida na kadhalika.
Katika soka, sasa tuna John Raphael Bocco, Mtanzania ambaye anaongoza kwa kufunga mabao mengi zaidi katika Ligi Kuu Bara.
Bocco amefunga mabao zaidi ya 100 na mengi amefunga akiwa na Azam FC ambayo si Simba wala Yanga kama ambavyo imezoeleka mashujaa wengi wa soka la Tanzania hutokea katika klabu hizo mbili kubwa.
Akiwa Azam FC, Bocco alipanda nayo daraja hadi kuiwezesha kuwa bingwa mara moja wa Ligi Kuu Bara, bingwa wa Kombe la Kagame lakini makombe kadhaa yakiwemo yale ya Mapinduzi.
Wakati ameamua kujiunga na Simba, gumzo lilikuwa namna alivyokosea na kadhalika. Taratibu alituonyesha uwezo wake haukuwa wa kubahatisha na unaona baada ya siku chache amekuwa nahodha wa Simba ambaye anaongoza gurudumu sahihi.
Bocco anaiongoza Simba katika njia sahihi, njia iliyo bora na tunaona kazi yake akiwa nahodha licha ya hadithi nyingi za kwamba ni mchezaji anayekosa sana mabao.
Hakuna mchezaji anayefunga kila nafasi anayoipata. Kama Bocco anakosa nyingi basi amefunga mabao mengi zaidi na ndiyo maana sasa ni mchezaji aliyefunga mabao mengi zaidi Ligi Kuu Bara.
Achana na hivyo, tumeona umuhimu wake katika mechi takriban tano za Simba ikiwemo ile kubwa dhidi ya Al Ahly. Bocco amefunga au kusababisha kupatikana kwa mabao ya ushindi yeye akiwa amechangia. Hili ni jambo kubwa kabisa.
Kikubwa cha kujiuliza ni kwamba katika wachezaji wa Kitanzania, yupi ambaye anaamini Bocco ndiye shujaa au mfano wa kuigwa? Au wachezaji wote wa Kitanzania wanawaangalia wachezaji wa nje tu kama akina Meddy Kagere, Emmanuel Okwi, Heritier Makambo?
Kama ni wahusika wa mpira, sisi waandishi wa habari na wadau wengine, tunauona ubora wa Bocco unaopaswa kupazwa zaidi na zaidi na kuwakumbusha wachezaji wengine wa Kitanzania kuwa na hamu ya kufikia hapo?
Angalia, wageni karibu wote wamekuwa wakija na kuondoka. Okwi pekee amekuwa akija na kurejea, lakini Bocco ameendelea kubaki palepale na kufanya kazi yake kwa ubora wa kiwango cha juu kabisa.
Bocco ameendelea kuwa bora kwa muda wote na tunapaswa kukubali kwamba kama amekuwa hivyo, basi Bocco ni bora na ubora huo unatokana na mambo mengi ambayo yamekuwa magumu kufanywa na wachezaji wa Kitanzania.
Kujihakikishia namba katika kikosi cha Simba katikati ya wageni walionunuliwa kwa bei kubwa si jambo dogo. Pia katikati ya wageni hao kuendelea kufanya vizuri kwa ubora wa juu kabisa si kitu kidogo.
Kuendelea kuwa alivyo Bocco inahitaji nguvu na uvumilivu wa juu sana kwa kuwa nidhamu ya ndani na nje ya uwanja, kulinda kiwango, kuwa ni mtu mwenye mwelekeo sahihi wa kutaka kufanya kilicho sahihi si jambo dogo na sote tunalijua hili kwa kuwa hata katika maisha ya kawaida linatakiwa kufanyika.
Bocco ni mfano wa kuigwa, Bocco ni shujaa katika taifa hili kwa kuwa hata atakapostaafu ataacha alama ya mfano mkubwa wa kuigwa ya aina ya wachezaji ambao tumekuwa nao.
Mchezaji ambaye pekee kwa muda mwingi amekuwa na ubora wa kuonyesha alichonacho mbele ya washindani ambao wengi ni wachezaji wa kigeni walionunuliwa au kulipwa mamilioni ya fedha.
Tuachane na ile kusubiri kulaumu pekee kwa kipindi tunaye Bocco na kusubiri kuanza kusifia siku akisema anastaafu na kuanza kuhesabu mafanikio yake wakati sasa tunayaona na hatuyatumii.
Wachezaji wa Kitanzania mnaochipukia au wale mlio ligi kuu mngependa kupata mafanikio, Bocco anaweza akawa ni black board (ubao) wenu wa mafunzo kwa kipindi hiki.
Angalieni nyendo zake, alipofikia haiwezi kuwa ni kwa njozi. Ukitaka kujua anafanyaje jifunze, jiulize na ingia "ndani" yake kujaribu viatu alivyovaa na ukiweza na kuongeza na nia na ubunifu wako, tutaitengenezea Tanzania wachezaji wengine bora wa kiwango wanaokuja huko mbele na wewe uliyeamua kufanya hivyo utakuwa mmoja wao.




0 Comments