Lolote liwe kudaadek! Kesho Jumamosi Simba itakuwa uwanjani kuivaa Al Ahly katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini habari nzuri ni kuwa bilionea wa Simba, Mohamed Dewji ‘Mo’ ni kama tayari amemaliza majukumu yake kwa asilimia kubwa na kilichobaki ni wachezaji wa Simba kumaliza kazi.
Mchezo huo umekuwa gumzo hasa kutokana na kiwango cha Simba katika siku za hivi karibuni kuonekana kuyumba lakini kuelekea mtanange huo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Borg El Arab ndani ya Mji wa Alexandria, maandalizi ya Simba yamekamilika kwa asilimia kubwa.
Ikiwa Simba itafanikiwa kupata ushindi kesho, utawawezesha kujikusanyia mamilioni ya fedha kutoka kwa Mo ambaye inadaiwa amewaahidi donge nono, hali ambayo imeongeza morali kwa asilimia kubwa kambini hapo.
Kwa mujibu wa Championi, Mtendaji Mkuu wa Simba (CEO), Crescentius Magori alisema kuwa, kupitia kwa Mwekezaji wao Mohammed Dewji 'Mo' endapo wachezaji hao watafanikiwa kupata ushindi katika mchezo huo wameandaliwa donge nono la fedha.
“Kuna ahadi kweli ya fedha ambayo tumeahidi wachezaji wetu kuwa tutawapatia endapo watapata ushindi katika mechi hiyo kama ambavyo tumekuwa tukifanya siku zote lakini kwa hii itakuwa tofauti kidogo.
“Kwa hiyo ni wajibu wao kupambana uwanjani ili kuhakikisha tunapata ushindi lakini pia kitita hicho cha fedha ambacho wao wanajua kuwa tumewaahidi kuwapatia mara tu watakaposhinda,” alisema Magori.
Hata hivyo, habari za kuaminika kutoka kwa mmoja wa wachezaji wa timu hiyo ambaye hakutaka kutajwa jina lake gazetini, zinasema kuwa, endapo watashinda mechi hiyo, kila mchezaji aliyecheza ataondoka na kikita cha Sh 4,000,000.
“Kabla ya kuja huku tulifanya kikao na uongozi na ukatuambia kuwa tukishinda kila mchezaji aliyecheza atapata Sh 4,000,000 na ambaye alikuwa benchi lakini hakucheza atachukua Sh 3,000,000.
“Wale ambao hawakusafiri na timu pia watapewa Sh 1,000,000 kila mmoja, kwa hiyo ni lazima tupambane uwanjani kwa nguvu zote ili kuhakikisha tunashinda.
“Lakini pia mbali na kupata fedha hizo, ushindi huo tutakaoupata utatusaidia kurudisha imani kwa mashabiki wetu ambayo hivi karibuni walituchukia kutokana na matokeo mabaya tuliyoyapata baada ya kufungwa mabao 5-0 na AS Vita ya DR Congo, lakini kiwango cha chini tulichokionyesha kwenye michuano ya SportPesa,” alisema mchezaji huyo.
0 Comments