Windows

MC MAARUFU BONGO AKWAA SKENDO YA UTAPELI


PAMELA Mboma ‘Mc Pam Tony’ ambaye ni mshereheshaji wa kwenye maharusi na shughuli mbalimbali, amekwaa skendo ya kudaiwa kutapeli kiasi cha shilingi milioni moja, alizokopa tangu Machi 3, 2016 kwa makubaliano ya kulipa ndani ya mwaka mmoja, pamoja na riba ya ya asilimia 20.

Kwa mujibu wa chanzo chetu, MC huyo alikopa fedha hizo kutoka kwa mjasiriamali mmoja anayeishi Bagamoyo ambapo siku za kulipa mkopo huo zilipowadia, MC huyo alianza kumpiga danadana, mara hapokei simu, akipokea anatoa visingizo lukuki na mwisho, simu yake ilikuwa haipatikani hewani.

“Mbali na U-MC, huyu dada pia ni mjasiriamali, ukiingia kwenye mitandao kama Facebook utaona anaposti kuhusu biashara zake, anatumia jina la Pam Tony huko Facebook.

“Sasa cha ajabu, na yeye inapotokea mteja wake anamzungusha fedha zake, basi humsimanga kwa maneno ya kuudhi na kuandika habari zake mitandaoni, anajifanya na yeye ni msafi sana, amesahau kwamba ametapeli zaidi ya shilingi milioni moja,” kilisema chanzo hicho.

Baada ya kupokea mdai hayo, gazeti hili liliwasiliana na mjasiriamali ambaye ndiye anayedaiwa kumkopesha MC huyo, ambaye kwa masikitiko makubwa alieleza kwamba ni kweli alimuamini na kumkopesha kiasi hicho kwa makubaliano ya kurejesha ndani ya miezi kumi na mbili pamoja na riba ya asilimia 20.

Akaongeza kwamba siku za marejesho zilipofika kama walivyoandikishiana kwenye mkataba, MC huyo aliingia mitini na amekuwa akiendelea kumsumbua kwa kipindi chote hicho akiwa hajalipa hata shilingi kumi.

“Tuliandikishiana mkataba kabisa na akakiri kwa maandishi na kuweka saini yake, sasa nashangaa anapoleta usanii. Nafikiria kulipeleka suala hili kwenye vyombo vya sheria, usawa huu mtu anakutapeli shilingi milioni moja kweli?

“Simu zangu mwanzo alikuwa hapokei baadaye akaamua na kubadili namba kabisa. Hili ni jambo lisilokubalika. Nimempa muda wa kutosha lakini kwa sababu anajifanya yeye ni mjanja, basi tutakutana mbele ya sheria,” alisema.


Baada ya kujiridhisha kuhusu madai hayo, ikiwa ni pamoja na kuona nakala ya mkataba wa mkopo aliosaini MC huyo, mwandishi wetu alimtafuta MC huyo kupitia namba za simu alizoweka kwenye mitandao kwa ajili ya kuwasiliana na wateja wake.

Alipopatikana kwa mara ya kwanza na kusomewa ‘mashtaka’ yake, alimwambia mwandishi wetu kwamba yupo kwenye kivuko, atampigia mwandishi wetu akishavuka. Hata hivyo, mwandishi wetu alisubiri kupigiwa na MC huyo bila mafanikio.

Alipopigiwa kwa mara nyingine, simu yake ilikuwa ikiita bila kupokelewa, hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maandishi na kusomewa tena kuhusu madai hayo, hakujibu chochote licha ya ujumbe kuonesha kwamba umemfikia.



Post a Comment

0 Comments