

KIKOSI cha Mashujaa FC ambacho kiliwaondoa Simba kwenye kombe la Shirikisho Uwanja wa Taifa, leo kitakuwa kazini kumenyana na Polisi Tanzania kwenye mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza utakaochezwa Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.
Kocha wa Mashujaa FC, Atuga Manyudo amesema wapo tayari kwa ushindani mbele ya wapinzani wao Polisi Tanzania watawavaa kwa ushujaa.
"Sisi ni mashujaa tunataka tuonyeshe ushujaa, mipango yetu ipo vizuri tunasubiri tu wakati ilitufanye kazi yetu, mpira ni mbinu sina mashaka na mbinu zangu," alisema.
Ofisa Habari wa Polisi Tanzania, Frank Geofrey amesema kundi walilopo ni gumu watajitahidi kupata matokeo ili watimize malengo ya kushiriki Ligi Kuu Bara.
Mbali na mchezo huo pia michezo mingine leo itakuwa ni kati ya Kiluvya United dhidi ya Ashanti, Mufindi dhidi ya Mawenzi Market, Njombe Mji dhidi ya Namungo, Reha dhidi ya Majimaji, Mlale dhidi ya Friends Rangers, Boma dhidi ya Transit Camp.
Rhino Rangers dhidi ya Arusha United, Green Warriors dhidi ya Mgambo Shooting na Arusha FC dhidi ya Geita Gold.



0 Comments