

Mabosi wa Simba wameweka bayana kwamba kwa sasa wanasubiri majibu kutoka kwa viongozi wa timu ya AFC Eskilstuna ili kujua hatima ya kiungo wao, Said Ndemla.
Ndemla kwa wiki mbili sasa aliondoka ndani ya kikosi hicho na kuelekea Sweden kwa ajili ya kufanya majaribio ndani ya kikosi cha Esklistuna ambacho Mtanzania Thomas Ulimwengu aliwahi kukichezea.
Mratibu wa Simba, Abbas Ally amesema wanawasubiri viongozi hao wa AFC Eskilstuna inayoshiriki ligi daraja la kwanza nchini humo, wawatumie majibu ya Ndemla kisha ndiyo wajue wanachukua maamuzi gani juu ya kiungo huyo.
“Kwa sasa kikubwa kinachosubiriwa ni majibu kutoka kwa wenzetu AFC Eskilstuna baada ya Ndemla kwenda huko na kurudi hapa nchini.
“Sisi hatujui chochote kilichotokea kwenye majaribio yake zaidi ya wao ambao ndiyo wana majibu kamili, wakishatuma majibu ndiyo viongozi wataamua sasa juu yake,” alisema Abbas.




0 Comments