MWENYEKITI wa Chama cha waamuzi Tanzania, Salum Chama amewataka viongozi wa timu kuacha tabia za kuwatupia mzigo wa lawama waamuzi pale timu zake zinaposhindwa kupata matokeo uwanjani.
Mzunguko wa pili timu nyingi zimekuwa zikitoa malalamiko yao kwa waamuzi kushindwa kumudu kufuata sheria 17 hali inayofanya washindwe kupata matokeo.
Chama amesema kuwa viongozi wengi wanashindwa kutambua kwamba waamuzi wanapewa semina na wanajua wajibu wao hali inayowafanya watafute sababu pale wanaposhindwa.
"Wengi wakishindwa kupata matokeo uwanjani wanakimbilia kuwapa lawama waamuzi, ila hilo sio sawa wanatakiwa waangalie wao huwa inakuaje pale ambapo wanapata matokeo? mbona wanakaa kimya, Chama huwa kinatoa adhabu kwa waamuzi wanaoshindwa kumudu mchezo.
"Kuna sababu ambazo zinawaponza washindwe kupata matokeo mbali na waamuzi ambazo ni pamoja na kambi, mishahara, chakula, pia kuwajenga kisaikolojia, mwamuzi anaweza kuchangia kiasi kidogo maana naye ni binadamu," amesema Chama.
Timu ambazo zilishusha lawama kwa waamuzi ni pamoja na Yanga baada ya kutoa sare na Coastal Union, Azam FC baada ya kutoa sare na Coastal Union, JKT Tanzania baada ya kupoteza mbele ya Alliance.
0 Comments