

Kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mohammed Issa ‘Banka’ ameweka bayana baada ya kuanza kuitumikia timu hiyo hakuna nyota ambaye anaweza kumuweka nje.
Banka aliyetua Yanga akitokea Mtibwa Sugar, Jumapili iliyopita kwa mara ya kwanza aliitumikia timu hiyo ikiwa ni baada ya kumaliza kifungo chake cha miezi 14 alichofungiwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kupitia Kamati ya Kuzuia na Kupambana na dawa zisizoruhusiwa michezoni ya Kanda ya Tano Afrika (Rado).
Kwa mara ya kwanza Banka aliingia uwanjani kuitumikia Yanga kwenye mechi dhidi ya JKT Tanzania akichukua nafasi ya Mrisho Ngassa.
Kiungo huyo anayevaa jezi namba 8, amesema baada ya kuanza majukumu ndani ya kikosi hicho atapambana na nyota yeyote ndani ya kikosi hicho litakapokuja suala la kugombania namba.
“Nafurahia kwanza kwa kupata nafasi ya kuitumikia timu yangu lakini pia nimejisikia raha.
“Kuhusu suala la namba hapa, kwangu nitapambana na mtu yeyote yule bila ya kujali ni nani lakini pia nitakuwa tayari kucheza na mtu yeyote nitakayepangwa naye kwenye eneo hili la kiungo,” alisema kiungo huyo Mzanzibar.




0 Comments