UONGOZI wa Alliance FC umesema kuwa kesho itakuwa ngumu kwa kikosi cha Lipuli ya Matola kupenya kwenye machinjio ya Uwanja wa Nyamagana mkoni Mwanza kwa kuwa tayari wamepata mbinu za kuingamiza pamoja na uzoefu kwa michezo yao iliyopita.
Alliance ambao wamepanda daraja msimu huu wameanza kurejea kwenye ushindani licha ya kufungwa na timu zote kubwa ikiwa ni pamoja na Simba na Yanga.
Ofisa Habari wa Alliance, James Mwafulango amesema mwendo walionao Alliance sasa ni kusambaza misumari ya moto hivyo Lipuli wajiandae kisaikolojia kupokea wanachokitaka.
"Kwa sasa naweza kusema kwetu sisi gari limewaka tutatumia vema Uwanja wa nyumbani kupata matokeo kwenye mchezo wetu wa Ligi Kuu dhidi ya Lipuli.
"Tunaiheshimu timu ya Lipuli tunaiheshimu, mchezo utakuwa mkubwa ila kikubwa hesabu zetu ni kupata matokeo kwenye uwanja wetu wa nyumbani, mashabiki watupe sapoti," alisema Mwafulango.
Alliance inashika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kucheza michezo 23 imejikusanyia pointi 28.
0 Comments