


LICHA ya kukubali kipigo cha kwanza kutoka kwa klabu ya Stand United, Kocha wa Yanga Mwinyi Zahera amesema hakuona maajabu yoyote kutoka kwa timu hiyo kwani walicheza mpira wa kawaida.
Juzi Yanga ilikubali kipigo cha bao 1-0 kutoka kwa Stand kwenye uwanja wa Kambarage Shinyanga , ikiwa ni kipigo cha kwanza msimu huu wa Ligi Kuu Bara kwa vinara hao wa ligi hiyo. Kocha huyo alisema wapinzani walikuwa wa kawaida na hawakutengeneza nafasi nyingi kama walivyofanya wao isipokuwa ilikuwa bahati yao baada ya kufunga bao hilo katika dakika za lala salama.
“Sikuona kitu cha ajabu wamefanya, hawakutengeneza nafasi ila wameshinda kwa bahati tu, sisi tumepata nafasi karibu mara tatu hatujaingiza goli,”alisema Mwinyi Zahera.
Nyota na nahodha wa timu hiyo Ibrahim Ajib alisema kuna baadhi ya makosa yaliyofanyika yaliyosababisha kupoteza mchezo huo na kusisitiza kuwa kocha Zahera ameona makosa hayo na atayafanyia kazi.
“Tumepoteza lakini michezo ipo mingi, tulijitahidi ila bahati haikuwa yetu, nina imani michezo ijayo tutafanya vizuri,”alisema Ajib.
Pamoja na kupoteza mchezo huo, Yanga bado inaongoza ligi kwa pointi 54, ikiwa imecheza michezo 19 Azam inashika nafasi ya pili ikiwa na pointi 41 na KMC ikishika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 34 baada ya kucheza mechi 22.



0 Comments