Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo wa wajumbe wa Bodi ya Mishahara na Maslahi katika Utumishi wa Umma na ameitaka ifanye kazi kwa weledi.
Ameiagiza ifanye marekebisho ya maslahi kulingana na mazingira ya mtumishi, akitolea mfano kada za elimu, afya, kilimo na mifugo ili yalingane na kazi wanazozifanya.
Amekutana na wajumbe wa bodi hiyo ,Januari 24, 2019 katika kikao kilichofanyika kwenye makazi ya Waziri Mkuu Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amesema Serikali ina nia njema ya kuhakikisha mishara na maslahi ya watumishi wa umma nchini yanaboreshwa, hivyo ameiagiza bodi hiyo ifanye kazi kwa bidii.
Amesema Serikali imeunda bodi hiyo ili kupata ushauri utakaotokana na tathmini sahihi ya nini Serikali inatakakiwa kufanya ili kuboresha utendaji wa watumishi wa umma nchini.
Serikali inaimani kubwa na wajumbe wote wa bodi hiyo kutokana na uzoefu walionao kwenye utumishi wa umma.
“Tunataka muongozo mzuri wa kuwafanya watumishi wa umma wafanye kazi yao kwa waledi bila ya kuwa na vishawishi vya aina yoyote ikiwemo kuomba na kupokea rushwa.”
Amesema Serikali inataka kila mtumishi wa umma anawajibika ipasavyo katika kuwatumikia wananchi mambo ambayo yatakuwa yameimarishwa kutokana na upatikanaji wa maslahi mazuri.
0 Comments