MKURUGENZI wa utawala na udhibiti wa SportPesa, Tarimba Abbasi, amezitaka klabu za Simba na Yanga kuacha masihara na badala yake kuhakikisha wanachukua ubingwa wa SportPesa Super Cup.
Kauli hiyo ameitoa leo katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Michuano hiyo inatarajiwa kuanza kutimua vumbi kesho jijini Dar inahusisha jumla ya timu nane nne za nchini Tanzania ambazo ni Simba, Yanga,Mbao na Singida United na za kutoka Kenya ni Gor Mahia ambaye ni bingwa mtetezi, AFC Leopard, Bandari na KK Sharks.
"Haiwezekani tena safari hii ubingwa wa michuano hii uende Kenya kama ilivyofanyika miaka miwili iliyopita, hivyo ni lazima timu za nchini kupambana kuhakikisha wanaubakisha ubingwa hapa nchini.
" Tayari nimekutana na viongozi wa Simba, Yanga, Mbao FC na Singida Utd nikiwasisitizia ubingwa ubaki nyumbani.
"Nimewaambia waache mzaha kabisa kwa kutumia wachezaji wa vikosi vya pili na badala yake kuwatumia wale wa kikosi cha kwanza.
"Mara kadhaa tumeziona Simba na Yanga wakitumia wachezaji wa kikosi cha pili, hivyo mwaka huu hatutaki kitu hicho kitokee kikubwa tunataka ubingwa," alisema Tarimba.
Bingwa wa michuano hii anatarajiwa kujichotea dola elfu 30 (Shilingi milioni 70).
0 Comments