Windows

TAKUKURU yashinda kesi saba na kufungua mpya nane


Na James Timber, Mwanza

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mwanza imeshinda kesi saba na kufungua kesi mpya nane mahakamani katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba 2018 mwaka jana.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Kaimu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mwanza Emmanuel Stenga amesema kuwa katika kipindi hicho jumla ya kesi 13 zimetolewa maamuzi, na upande wa Jamhuri imeshinda kesi saba na kesi sita zimeshindwa na kesi tano kati ya hizo zimekatiwa rufaa.

Stenga amesema kuwa katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba, jumla ya malalamiko 135 yamepokelewa, kati ya malalamiko hayo serikali za mitaa zinaongoza kwa kuwa na jumla ya malalamiko 31 ikifuatiwa na idara ya afya 18, elimu 14, polisi 13, ardhi 12, maliasili na uvuvi nane, taasisi za fedha saba, na idara nyingine malalamiko 20.

Ameeleza kuwa tafiti ndogo saba zimefanyika na vikao vya wadau vimeitishwa ili kufanya udhibiti na uzibaji wa mianya ya rushwa iliyobainishwa na Idara na taasisi zilizohusika ni Fedha, Polisi, Mahakama, Ujenzi, na Uvuvi.

"TAKUKURU imefanya ukaguzi wa miradi 26 ya maendeleo yenye thamani ya shilingi Bilioni 31,671,018,432 ambapo miradi nane imekamilika na miradi 18 iko kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji na hakuna mradi ulioonekana na kasoro, amesema.

Aidha aliongeza kuwa TAKUKURU imekusudiwa kuongeza kasi ya ufuatiliaji wa karibu na ukaguzi wa miradi ya maendeleo, lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa thamani ya fedha inapatikana kwa kila mradi na inatekelezwa katika ubora uliokusudiwa ikiwa ni pamoja na kudhibiti vitendo vya rushwa na kuokoa fedha za serikali na wafadhili zisifanyiwe ubadhirifu.



Post a Comment

0 Comments