Na Saleh Ally
MICHUANO SportPesa SuperCup, imeanza kwa raha ya aina yake. Sasa iko katika hatua ya nusu fainali ikiwa na mgawanyiko bomba kabisa.
Mgawanyiko huu ni ule unatokana na uhalisia ambao unaongeza utamu wa mashindano yenyewe kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Nazungumzia kuongezeka kwa utamu kwa kuwa michuano hiyo ilianza na timu nane, kukiwa na mgawanyiko wa nusu kwa nusu kwa kuwa timu nne zinatokea Tanzania ambao ni wenyeji na nne zinatokea Kenya.
Kutoka Tanzania ni Simba, Yanga, Singida United na Mbao FC na kutoka Kenya ni Gor Mahia, FC Leopards, Kariobangi Sharks na Bandari.
Baada ya siku mbili za mashindano hayo, mambo yako hivi, mgawanyiko unaendelea kuwa nusu kwa nusu kwa kuwa timu mbili za Tanzania zimezing'oa mbili kutoka Kenya na Wakenya nao wakafanya hivyohivyo.
Leo kuna nusu fainali, mechi mbili zinazohusisha timu nne, mbili kutoka Tanzania dhidi ya mbili kutoka Kenya na hii inazidi kuongeza utamu wa mashindano yenyewe.
Utamu unazidi kunoga kwa kuwa ushindani unakuwa ni ule wa kitaifa na kama nilivyotangulia kuandika kwamba Watanzania wamechoshwa na utawala wa Wakenya katika michuano ya SportPesa Super Cup.
Mara ya kwanza fainali ilikuwa ni AFC Leopards dhidi ya Gor Mahia ambao walishinda na kubeba kombe hilo kwenye ardhi ya Tanzania na lilipokwenda kwao wakakutana fainali na Simba, wakabeba tena kombe hilo.
Safari hii Gor Mahia wamekutana na Mbao FC na wameng'oka mapema. Na si wao tu, maana siku mbili za michuano hiyo zimeondoka na vigogo watatu wa soka la Afrika Mashariki.
Kwa Tanzania vigogo wanajulikana, Simba na Yanga, Kenya ni Gor Mahia na Leopards. Lakini hatua ya nusu fainali unakutana na kigogo mmoja tu aliyebaki ambaye ni Simba.
Kuondoka kwa vigogo watatu kati ya wanne walio mashindanoni maana yake mashindano yana mwendo tofauti na ule ambao ungetarajiwa na wengi.
Kawaida ungetarajia kuona nusu fainali angalau ina vigogo watatu na idadi ya chini kabisa angalau basi wawili na si mmoja kama ilivyo sasa.
Kama vigogo wanang'olewa mapema, maana yake timu ambazo si vigogo zimejipanga na zinaonekana kuelewa umuhimu au ukubwa wa michuano ya SportPesa Super Cup.
Michuano hiyo ndiyo inafanyika msimu wa tatu, lakini zawadi yake ya dola 30,000 kwa kucheza mechi nne pekee, si haba hata kidogo. Lakini ile bonus ya kucheza na timu kubwa kama Everton, si jambo dogo. Everton inashiriki Ligi Kuu England ambayo ni kubwa zaidi duniani. Hili si jambo la kupuuzia.
Timu zilizoonekana ndogo kama Mbao FC, Bandari au Kariobang wanaonekana wamelielewa hilo na walilifanyia kazi kuhakikisha wanafikia katika hatua nzuri kuanzia fainali au kulibeba kombe hilo.
Supraizi yao inaifanya michuano hiyo kuongeza thamani kwa maana ya haki na hakuna timu inayobebwa kwa ukubwa au jina lake. Kwamba kila upande lazima ujipange kufanya sahihi.
Hali inavyokwenda pia kunaweza kuwa na mshangao mwishoni kama kigogo mmoja hatajipanga vizuri. Simba lazima ajue Bandari wanaotokea Pwani ya Mombasa watataka kucheza fainali na tayari wameona inawezekana vigogo kuchezea kichapo, kwanini wao washindwe.
Kama Bandari watakwenda fainali, maana yake itakuwa ni fainali isiyotarajiwa kwa kuwa tayari upande wa nusu fainali ya Kariobangi na Mbao FC itapeleka fainali timu ambayo haikutarajiwa.
Hivyo, kuonyesha waliotarajiwa, kuwapa Watanzania matumaini ya kulibakiza kombe ni lazima Simba itinge fainali na kama Mbao FC nao watakuwa wameingia fainali, uhakika kuwa limebaki Tanzania kwa mara ya kwanza utakuwa umetimia.
Kama Mbao watafanya mzaha na Simba akajiamini kupindukia kwa mara ya tatu hata kama halijachukuliwa na Gor Mahia, basi litakwenda tena Kenya, jambo ambalo kwa wapenda mpira wa Tanzania litakuwa ni sawa na unyanyasaji.
Hadi sasa, waamuzi wanaochezesha michuano hiyo wanastahili pongezi kwa kuwa wanaifanya kazi yao vizuri ndiyo maana unaona imefikia hivi.
Kuna makosa kadhaa yametokea lakini yanaashiria uanadamu wa kawaida, jambo ambalo pia halijawa kwa kiwango cha juu ambacho kinafikia hadi kukwaza au kukera kwa kupindukia.
0 Comments